Monday, December 22, 2008

Yanga yatolewa kwa kura kombe la Tusker

MABINGWA watetezi wa kombe la Michuano ya Tusker, Yanga, jana walitolewa kwenye michuano hiyo kwa kura baada ya timu zote tatu kuwa sawa kwa kila kitu katika kundi A.

Matokeo hayo, yakatoa ugumu wa timu gani iondoke kati ya hizo tatu, hivyo utaratibu wa kura ukatumika ili kupata timu ya kung’oka huku mbili zikisonga mbele kwa hatua ya robo fainali.

Katika kura hizo zilizopigwa makao makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Karume jijini Dar es Salaam, URA ya Uganda iliibuka mshindi wa kwanza wa kundi A huku Mtibwa Sugar ikiwa ya pili.

Wakati URA na Mtibwa Sugar zikisonga mbele, Mabingwa watetezi Yanga, waliaga baada ya kuchagua fungu la kukosa katika upigaji wa kura kwa kuchagua karatasi iliyoandikwa nje (out).

Kwa mujibu wa taratibu za jana, karatasi ziliandikwa namba 1 na 2 huku nyingine ikiandikwa out, vilitumbukizwa katika bahasha ambako viongozi wa timu walitakiwa kuchagua.

Yanga ikiwakilishwa na Katibu wa Kamati ya Mashindano, Emmanuel Mpangala, alikuwa wa kwanza kuchagua kikaratasi na alipofungua, karatasi ilisomeka out.

Wakati Mpangala akiokota ‘out’, Godfrey Kalimba ambaye ni Daktari wa timu ya Mtibwa Sugar, alikuwa wa mwisho kuokota karatasi na alipofungua, alikuta namba 2, ikiwa na maana mshindi wa pili.

Kilichofuata, ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Tusker, Salum Madadi kuzitangaza URA na Mtibwa Sugar kwamba ndizo zitakaocheza hatua a nusu fainali ya michuano hiyo.

Madadi alisema, hatua iliyofikiwa ya kupiga kura hizo, ni kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo kwamba, timu zikilingana kwa kila kitu, kitakachofuata, ni kupigwa kura.

Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Fredrick Mwakalebela, alisema kura zimepigwa katika hali ya uwazi na timu zote zimeridhika na matokeo hayo.

Alisema uamuzi uliofanyika kutoka kwa Kamati ya Mashindano, ni sahihi kulingana na kanuni na katiba ya michuano hiyo.

Kwa matokeo hayo, mshindi wa kwanza kundi A, atakumbana na mshindi wa pili wa kundi B huku mshindi wa pili wa kundi A atakutana na mshindi wa kwanza wa Kundi B kwenye mechi zitakazopigwa kesho na keshokutwa.



No comments:

Post a Comment