Sunday, December 7, 2008

Masha ampa siku saba Mengi

WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, amempa siku saba Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, kuthibitisha madai ya kutishiwa kuuawa na suala kwamba kuna waziri anayepanga kumfilisi.

Pia amesema kuwa madai hayo ya Mengi ni mazito na umefika wakati ayathibitishe tuhuma hizo, kwani hakumtaja waziri yeyote wakati anazungumza na waandishi wa habari.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi Dar es Salaam, Masha alisema atamwandikia rasmi barua Mengi ya kutaka kuthibitisha madai hayo.

“Leo hii nitamwandikia ingawa mpaka sasa sijamwandikia barua, ili ndani ya siku saba kuanzia leo (juzi) awe amethibitisha,” alisema Masha.

Masha pia alizungumzia suala hilo juzi asubuhi wakati akizungumza kwenye kipindi cha Jambo Tanzania cha Televisheni ya TBC1.

Alisema Mengi licha ya kuwa na uhuru wa kutoa maoni yake, lakini tayari amejenga hisia kwenye akili za wananchi kuwa kuna jambo la namna hiyo, hivyo anapaswa kulithibitisha.

Masha alisema iwapo Mengi hatathibitisha madai hayo atachukuliwa hatua za kisheria ingawa hakufafanua hatua hizo.

Hata hivyo alisema madai ya Mengi kutishiwa kwa kutumiwa ujumbe mfupi wa simu, vyombo vya dola vitayachunguza na wale watakaobainika kufanya hivyo lazima nao wachukuliwe hatua.

Alisema pamoja na hayo suala la yeye kutaka abambikiwe kesi, halihitaji uchunguzi na ndio maana serikali inampa siku saba awe ametoa ushahidi wake.

Alisisitiza kuwa iwapo Mfanyabiashara huyo hatapeleka uthibitisho wowote, na kwa kuwa nchi inaongozwa kwa utawala wa sheria, mamlaka zitaangalia taratibu zipi zitumike ili mambo ya namna hiyo yasiendelezwe.

Juzi, gazeti la Uhuru lilimkariri Kaimu Kamishna wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Evarist Mangala akisema Jeshi la Polisi halina taarifa yoyote kuhusu madai hayo ya Mengi kutishiwa kuuawa.

Jumatano wiki hii, Mengi aliitisha mkutano na wanahabari na kudai kuna waziri mmoja kijana ambaye anaongoza wizara nyeti, amependekeza hivi karibuni katika moja ya vikao ili Mengi abambikiziwe kodi bandia ya kiasi kikubwa atakachoshindwa kulipa na hatimaye afilisiwe.

Aidha katika mkutano huo alisema amekuwa akipokea vitisho vya kuuawa kutoka kwa watu wasiojulikana kupitia ujumbe mfupi wa simu yake ambao wanadai amezidi kushabikia kwa kupiga vita ufisadi.

No comments:

Post a Comment