Thursday, December 25, 2008

'Kiongozi' wa Guinea atajwa

Majeshi yaliyochukua uongozi nchini Guinea yamemtaja Kapteni Moussa Dadis Camara kuwa ndiye kiongozi wa utawala wa kijeshi, huku amri ya kutotembea usiku ikitangazwa pia.

Katika hatua nyingine Umoja wa kiuchumi wa Afrika Magharibi Ecowas umesema utatuma ujumbe nchini Guinea kesho kujaribu kuwashawishi wanajeshi kurejesha utawala wa kikatiba.

Wakati huohuo maafisa wa kijeshi waliochukua madaraka nchini Guinea siku ya Jumatatu wamewatuhumu baadhi ya maafisa wa kijeshi wanaotii serikali iliyokuwa madarakani, kwa kuingiza mamluki nchini humo.

Wamesema wale wanaohusika na kuingiza majeshi kutoka nje ya nchi watawajibika kwa lolote litakalotokea.

Viongozi wa mapinduzi, waliochukua madaraka saa chache baada ya rais wa nchi hiyo Lansana Conte kufariki dunia, wameahidi kuandaa uchaguzi katika kipindi cha miaka miwili.

Katika matangazo ya televisheni ya taifa, wametaka wananchi wa Guinea kutoingia mitaani na kufanya maandamano.

Umoja wa Afrika, ambao umelaani mapinduzi hayo, unafanya mkutano wa dharura kujadili yanayotokea Guinea.


Source: BBC

No comments:

Post a Comment