Sunday, December 21, 2008

Evander Holyfield ashindwa kwa pointi na Valuev

Ndoto ya Evander Holyfield kuwa bingwa wa dunia mzee kuliko wote iliyeyuka baada ya kutandikwa na mrusi Nikolai Valuev katika kugombea ubingwa mkanda wa WBA.

Nikolai Valuev, jitu la miraba saba, mrefu na mzito kuliko mabingwa wote waliowahi kutokea kwenye ndondi alifanikiwa kumshinda Holyfield kwa kura za majaji katika pambano hilo la raundi 12.

Valuev alipata tabu katika jitihada zake za kumdondosha Holyfield raundi za mwanzo lakini akafanikiwa kumdhibiti vyema raundi za mwisho Holyfield alipoanza kuchoka.

Marefa wawili walimpa ushindi Valuev kwa pointi 116-112 na 115-114 wakati refa mmoja aliamua pambano hilo kuwa ni sare.

Evander mwenye miaka 46 alisema baada ya pambano hilo "Nilifikiria nimefanya kila kitu cha kuniwezesha kushinda,sasa inanibidi niende nyumbani nikafikirie hatima yangu ya baadae".

Holyfield (42-10-2) hakuingia kwenye ulingo tangu alipopewa kisago cha nguvu na Sultan Ibrahimov ambaye alikuja kuwa bingwa wa WBO zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

Watu wengi walimkosoa Holyfield kwa kuweka maisha yake hatarini kwa kurudi tena ulingoni wakati umri wake ukiwa umeenda sana.

Kocha wa Valuev alisema baada ya pambano hilo "Valuev alianza vizuri raundi za mwanzo lakini raundi za mwisho alikuwa akidansi tu , marefa wangeweza hata kuamua kuwa pambano hili kuwa ni sare".

Mshindi wa pambano hilo Valuev amejishindia kitita cha Euro milioni moja wakata Evander Holyfield amejifuta machozi na Euro laki tano.

Picha nyengine zaidi za pambano hilo:













No comments:

Post a Comment