Monday, December 8, 2008

Ghana wachagua Rais mpya leo

Wapiga kura 12,000,000 wamejitokeza kuchagua rais mpya na wabunge 230 katika uchaguzi mkubwa unaofanyika leo katika vituo 21,000 vya kupigia kura.

Wananchi katika nchi hiyo yenye watu milioni 22 wanaingia kuchagua raisi mpya katika uchaguzi wa tano wa kidemokrasia katika miaka 16 tangu nchi hiyo ilipoachana na utawala wa kijeshi.

Vyama vinane vinashiriki katika uchaguzi huo lakini maoni ya watazamaji wa nje yanaonyesha upinzani wa karibu kati ya chama tawala NPP na chama cha upinzani cha NDC. Mshindi wa uchaguzi huo anatakiwa apate zaidi ya asilimia 50 ya kura zote na kura moja ya ziada.

Wagombea uraisi katika uchaguzi huu ni Waziri wa mambo ya nje wa zamani Nana Akufo-Addo anayegombea kupitia chama cha NPP, makamu wa raisi Prof. John Evans Atta-Mills wa NDC, Dr Paa Kwesi Nduom wa CPP ,Dr Edward Mahama wa PNC, T.N Ward Brew wa DPP, Emmanuel Ansah-Antwi wa DFP, Kwabena Adjei wa RPD na mgombea huru Kwesi Amoafo-Yeboah.

Macho ya dunia yataelekezwa katika nchi hii ambayo hivi karibuni ilitangaza kugundulika kwa kiasi kikubwa cha mafuta, baada ya masaa 78 wakati matokeo ya uchaguzi huu yatakapotangazwa.

No comments:

Post a Comment