Thursday, December 18, 2008

Kinara wa mauaji Rwanda ahukumiwa

Afisa wa zamani wa jeshi la Rwanda Theoneste Bagosora amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kupanga mauaji ya mwaka 1994 ya Rwanda.

Bagosora pamoja na washitakiwa wenzake wawili walipatikana na hatia na mahakama ya Umoja wa Mataifa ya uhalifu wa kivita ya kuongoza mauaji ya kuangamiza watu wa kabila la Watutsi pamoja na Wahutu wenye msimamo wa wastani.

Hii ni mara ya kwanza mahakama ya Rwanda kumtia hatiani mtu yeyote kwa kuhusika kupanga mauaji.

Zaidi ya watu 800,000 waliuawa nchini Rwanda katika wimbi hilo la mauaji ya kimbari.

Wengine waliohukumiwa na Bagosora, ni makamanda wawili wa zamani wa jeshi la Rwanda Anatole Nsegiyumva na Alloys Ntabakuze ambapo pia walipatikana na hatia ya kupanga mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita na wote wamehukumiwa kifungo cha maisha jela.

Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu inayosikiliza kesi za mauaji ya Rwanda
(ICTR), yenye makao yake Tanzania, ilikataa pingamizi la upande wa utetezi uliosema mauaji hayo hayakupangwa kwa hiyo si mauaji ya kuangamiza.

No comments:

Post a Comment