Saturday, December 13, 2008

Kupambana na uharamia waleta utata

Kamanda Mkuu wa jeshi la majini la Marekani katika Ghuba ya Aden na Bahari ya Hindi ameondoa matumaini uharamia kwenye pwani ya Somalia unaweza kutatuliwa kwa kushambulia vituo vyao vya nchi kavu.

Kamanda huyo Bill Gortney amesema sera kama hiyo itazuiwa na ugumu wa kuwatambua maharamia hao na hatari iliyopo ya kuwadhuru raia.

Badala yake amependekeza makampuni ya meli kuajiri walinzi wa usalama wenye silaha kulinda meli zao kutekwa nyara.

Kamanda Gortney alikuwa akizungumza katika siku ya kwanza ya mkutano juu ya usalama katika ghuba hiyo.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Robert Gates, amesema Marekani itafikiria tu kushambulia maeneo ya nchi kavu ya maharamia wa Somalia kama Marekani yenyewe ingekuwa na vifaa bora.

Amesema kampuni za meli lazima zichukue hatua za awali za usalama, ikiwa ni pamoja na kuongeza kasi wanapoona maharamia wakikaribia na kupandisha ngazi zao.

Mkutano wa masuala ya usalama unaofanyika Bahrain unahudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi 25.

No comments:

Post a Comment