Thursday, December 18, 2008

Yanga yaanza vizuri kombe la Tusker

Mabingwa watetezi Yanga jana walianza vizuri michuano ya Kombe la Tusker baada ya kuifunga Mamlaka ya Mapato ya Uganda, URA, kwa bao 1-0, katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Yanga ambayo kabla ya mchezo huo ilitamba kuibuka na ushindi mnono, iliandika bao hilo la ngama katika dakika ya 22 mfungaji akiwa ni Jerry Tegete aliyeunganisha wavuni mpira wa krosi uliochongwa na Shamte Ali.

Watoza Ushuru wa Uganda nusura wapate bao la kuongoza katika dakika ya 10 baada ya mchezaji wake Eric Obua kupiga mpira juu licha ya kuwa katika nafasi nzuri ya kufunga.

Mwamuzi Nicodemua Marina alishindwa kumuonyesha kadi Hamis Yusuph katika dakika ya 43 licha ya kumvuta jezi mchezaji wa Uganda aliyekuwa akienda golini kufunga bao.

URA walikosa tena bao katika dakika ya 52 baada ya Obua kupiga shuti pembeni ya lango baada ya mkwaju wa Patrick Ochan kupanguliwa na kipa wa Yanga Juma Kaseja na kurejea uwanjani.

Kocha wa URA Moses Masena alisema kuwa timu yake ilicheza vizuri lakini kosa moja walilofanya lilitumiwa vizuri na Yanga kujipatia bao hilo pekee lililowawezesha kuibuka na pointi tatu muhimu.

Timu hiyo hadi sasa imejikusanyia pointi tatu na tayari imemaliza mechi zake.

Naye kocha msaidizi wa Yanga, Spaso alisema kuwa timu yake haikucheza vizuri licha ya kuibuka na ushindi huo kutokana na baadhi ya wachezaji wake kutokuwa pamoja.

Alisema kuwa wachezaji wake wengine ni majeruhi, hivyo iliwabidi kuwachezesha wale ambao kwa muda mrefu hawajacheza.

Yanga:Juma Kaseja, Shadrack Nsajigwa, Abdul Ntiro, George Owino, Hamis Yusuph, Shamte, Castory Mumbala, Abdi Kassim, Ben Mwalala/Gaudence Mwaikimba (38), Jerry Tegete/Wisdom Dlovu (dk.74) na Amir Maftah/Kigi Makasi (51).

Ura:Abbey Dhaira, Sam Mubira, David Kyobe, John Karangwa, Joseph Owino, Manco Kawesa, Tonny Mawejje, Patric Ochan, Martin Muwanga/Henry Kiseka (dk 28), Ismail Kagozi na Eric Obua/Sadat Kaire (78).

No comments:

Post a Comment