Friday, December 5, 2008

Bao langu limetoka kwa Haruna Moshi: Ngassa

MSHAMBULIAJI wa timu ya soka ya Taifa ‘Taifa Stars’ Mrisho Ngassa amesema pamoja na kufunga bao la kuongoza katika mchezo wa juzi dhidi ya Sudan amedai hawezi kusahau mchango mkubwa kutoka kwa kiungo wa timu hiyo Haruna Moshi.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam, Ngassa alisema kuwa kiungo huyo ndiye aliyechangia ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya wapinzani wao Sudan katika mchezo wa juzi uliochezwa katika Uwanja Mkuu wa taifa.

Alisema mara nyingi pasi za kiungo huyo zilikuwa hazipotei kutokana na umakini wake uwanjani.

“Nilifurahi sana kufunga bao la kwanza lakini kilichonipa furaha zaidi ni jinsi Haruna Moshi alivyocheza siku ile kwa kiwango cha juu naweza kusema yeye ndiye alilishika dimba lote maana pasi zake zote ambazo alikuwa akizipiga zilikuwa na madhara kwa wapinzani,”alisema.

Alisema kwa uwezo ambao alionyesha kiungo huyo ulikuwa wa hali ya juu kitu ambacho kimewashangaza wengi ambao walifika kuangalia mchezo huo.

“Alikuwa chachu kwetu hata mwalimu hilo alisema tunashukuru kuwafunga wapinzani wetu hivyo hivyo tutaenda kufanya kwao wiki mbili baadae,”alisema.

Stars ambayo juzi iliweza kuutumia vyema uwanja wao wa nyumbani waliweza kuilaza Sudan mabao 3-1 ikiwa ni katika hatua za kutafuta kucheza fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza Ligi za ndani.

No comments:

Post a Comment