Thursday, December 25, 2008

Mtibwa yaingia fainali kombe la Tusker

Timu ya Mtibwa Sugar imewaondolea aibu Watanzania baada ya kutinga fainali ya Kombe la Tusker kwa kuwachapa Tusker ya Kenya kwa mabao 2-1 katika mechi ya nusu fainali.

Ushindi katika mechi hiyo ya nusu fainali ya pili iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam jana, umeiwezesha Mtibwa kuitoa kimasomaso Tanzania baada ya mabingwa watetezi Yanga na Simba waliopewa nafasi kubwa kutolewa mapema.

Mtibwa watakutana na timu ya Mamlaka ya Mapato (URA) ya Uganda keshokutwa katika mchezo wa fainali. Yanga walikuwa wa kwanza kuaga michuano hiyo kwa kura katika hatua ya makundi, wakati Simba walilala kwa mabao 2-1 dhidi ya URA katika mechi ya nusu fainali ya kwanza juzi.

Mtibwa kutoka Turiani Morogoro, walikuwa wa kwanza kuliona lango la wapinzani wao baada ya David Mwantobe kuachia shuti kali dakika ya 28. Noah Obichi aliisawazishia Tusker dakika ya 38 kwa njia ya penalti. Dakika ya 42 kipa wa Mtibwa, Shaaban Kado alifanya kazi ya ziada kuokoa hatari kwenye lango lake na kuwanyima wapinzani wao bao la kuongoza.

Hali hiyo ilifanya hadi mapumziko timu hizo kuwa sare ya bao 1-1 katika mchezo huo mkali. Kipindi cha pili kilianza kwa kasi zaidi huku kila timu ikiwania ushindi, lakini bahati iliangukia kwa Mtibwa dakika ya 48 baada ya Salum Swedi kuunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu ndogo uliochongwa na Uhuru Selemani.

Mchezaji wa Mtibwa, Rashidi Gumbo aliangushwa karibu na eneo la penalti la Tusker hivyo Mwamuzi Oden Mbaga kutoka Uganda kuamuru ipigwe adhabu hiyo iliyozaa matunda. Mtibwa ambao hawakupewa nafasi kubwa ya kufika fainali za michuano hiyo wameonyesha makali baada ya mchezo wa mwisho wa kundi A pia kuwalaza Yanga kwa bao 1-0 na kusababisha kura kupigwa ili kupata timu zitakazosonga mbele kutokana na timu zote kundi hilo ikiwemo URA kila mmoja kuwa na pointi 3 na bao moja.

Vijana hao wa Turiani wamepata nafasi ya kulipa kisasa kwa URA ambao waliwachapa kwa bao 1-0 katika mchezo wa ufunguzi wa michuano hiyo Desemba 15. Matokeo hayo yanaonyesha kundi A lilikuwa gumu zaidi kutokana na fainali kukutanisha timu zote za kundi hilo. Akizungumza baada ya mechi ya jana Kocha wa Mtibwa, Salim Mayanga alisema mchezo ulikuwa mgumu tofauti na walivyotegemea.

“Hatukutegemea upinzani mkali kama ilivyokuwa, sasa tutajipanga vizuri kwa ajili ya fainali,” alisema Mayanga. Naye kocha wa Tusker, James Nandwe alisema mchezo ulikuwa mgumu na kila mtu alikuwa akitafuta nafasi lakini wenzao walizitumia vyema. Nandwe alisema Mtibwa wamestahili kushinda kwani wameonyesha mchezo mzuri na kuimwagia sifa timu hiyo.

Kocha huyo alisema anajiandaa kukutana na Simba katika mechi ya kutafuta mshindi wa tatu itakayofanyika kesho kwenye uwanja huo na kuongeza kuwa atafanya mabadiliko kwa wachezaji kadhaa kwenye kikosi chake. Hata hivyo, kocha huyo alimlalamikia mwamuzi Mbaga kwa kutoongeza muda wa takribani dakika nne ambazo mchezo ulisitishwa kutokana na kipa wa Mtibwa, Shaaban Kado kuumia.







No comments:

Post a Comment