Tuesday, December 23, 2008

Nusu ya darasa la saba wafeli

Udhaifu wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) ulioanza mwaka 2002 umeendelea kuonekana baada ya nusu ya wanafunzi waliofanya mitihani ya kumaliza darasa la saba mwaka huu kufeli.

Kati ya wanafunzi 1,017,967 waliofanya mitihani ni wanafunzi 536,672 tu sawa na asilimia 52.73 waliofaulu, wakiwemo wasichana 229,476 sawa na asilimia 45.55 ya wasichana waliofanya mtihani na wavulana 307,196 ambao ni sawa na asilimia 59.75 ya wavulana waliofanya mtihani.

Matokeo haya ni kipimo cha pili cha MMEM baada karibu nusu ya wahitimu wa kwanza toka mpango huo uzinduliwe kufanya vibaya kwenye mtihani wa darasa la saba.

Katika matokeo ya darasa la saba mwaka jana, ni asilimia 54.18 ya wanafunzi 773,550 watainiwa waliofanya mtihani wa darasa la saba waliofaulu, hivyo mwaka huu kiwango cha ufaulu kimezidi kushuka kwa kuangalia asilimia.

Katika matokeo ya mwaka huu, Mkoa wa Dar es Salaam umeongoza kitaifa kwa kufaulisha asilimia 73.9, ikifuatiwa na Arusha, Iringa na Kagera.

Aidha, mikoa iliyofanya vibaya zaidi ni Shinyanga, Lindi, Mara na Tabora.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe, alisema mikoa yote nchini leo inatangaza matokeo yake na wanafunzi waliochaguliwa.

Matokeo hayo yanaonyesha kuwa karibu nusu ya wanafunzi waliofanya mitihani wamefeli na wengine wameshindwa kufanya vizuri katika masomo ya Hisabati na Kiingereza.

Waliofanya mitihani hiyo ni 1,017,969, lakini waliofaulu ni 536,672 na jumla ya waliofeli ni 481,193 wakiwemo wasichana 274,283 na wavulana 206, 910.

Waziri Maghembe alisema wanafunzi 433,260 sawa na asilimia 80.7 ya waliofaulu wamechaguliwa kuingia kidato cha kwanza kwa shule za sekondari za serikali.

Alisema kati ya wanafunzi waliochaguliwa wasichana ni 188,460 sawa na asilimia 82.13 ya wasichana waliofaulu na wavulana 244,800 sawa na asilimia 79. 69 ya wavulana waliofaulu.

Waziri alisema watahiniwa 102 waliofanya mitihani yao wakiwemo wasichana 41 na wavulana 61 wamefutiwa matokeo yao kwa sababu mbalimbali za udanganyifu katika mitihani hiyo.

Waziri alisema katika mtihani huo, ufaulu katika somo la Kiswahili umeshuka kwa asilimia 6.6 na Kingereza kwa asilimia 0.26, wakati ufaulu katika somo la Sayansi umepanda kwa asilimia 1.5, Maarifa kwa asilimia 4.6 na Hisabati kwa asilimia 0.6.

Kuhusu matokeo ya wenye ulemavu, Waziri alisema jumla ya wanafunzi 346 walifanya mitihani na kati yao wanafunzi 221 wamefaulu na kwamba wote wamechaguliwa kujiunga na sekondari.

Wanafunzi hao walifanya mitihani yao Septemba 10 na 11.

Akizungumzia matokeo hayo, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba alishtushwa na matokeo hayo na kusema kuwa wanaopaswa kuulizwa kuhusu kufeli huko ni watunga sera na wale wa mitaala.

Alisema kwa upande wao walimu wasitupiwe lawama kwani wamekuwa wakichapa kazi usiku na mchana tena kwa moyo.

Mukoba alisema kufeli huko hakuna uhusiano wowote na mgogoro baina ya CWT na serikali kwani wakati mgomo unaanza wanafunzi hao walishafanya mitihani yao.

``Kufeli huko kusihusishwe na mgomo maana walishafanya mitihani, labda wakifeli mwakani unaweza kusema ni kwasababu ya mgomo lakini si mwaka huu,`` alisema Mkoba.

Ripoti ya Shirika la Hakielimu ya mwaka 2005 kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Msingi (MMEM), ilisema kuwa wanafunzi wako wengi madarasani na madarasa yamejengwa kwa wingi, lakini vifaa vya kufundishia havipo.

Ilisema Tanzania itarajie kupata wahitimu wasio na sifa stahili kutokana na mfumo mbovu wa elimu uliopo.
Lengo la mpango wa MMEM ni kuandikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule, lakini ulundikwaji wa wanafunzi madarasani na ukosefu wa walimu zimekuwa ni changamoto toka mpango huo kuanzishwa.

Mbali na kuwa serikali inatoa zaidi ya asilimia 18 ya bajeti yote katika elimu.

Wataalam wa masuala ya elimu wamekuwa wakihoji juu ya mpango huo kutoa kipaumbele kuandikisha wanafunzi shuleni bila kujali ubora wa elimu inayotolewa.


Source: Nipashe

No comments:

Post a Comment