MAELFU ya wakazi wa jijij la Dar es Salaam jana waliacha shughuli zao kwa muda na kulijitokeza kuipokea timu ya soka ya taifa, Taifa Stars ilipokuwa ikirejea kutoka Khartoum, Sudan ilipofanikiwa kufuzu kucheza fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).
Mbali na kufuzu na kuvunja rekodi ya miaka 28 iliyopita, pia Stars imevunja mwiko wa Sudan wa kutofungwa katika uwanja wao wa nyumbani kwa miaka 13 baada ya kuitandika mabao 2-1, lakini pia katika mchezo wa awali uliofanyika katika Uwanja Mkuu wa Tanzania, Stars ilishinda kwa mabao 3-1, hivyo kusonga mbele kwa mabao 5-2. Stars iliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere saa 3:15 asubuhi ambapo nahodha wao Henry Joseph na msaidizi wake, Nadir Haroub 'Cannavaro' ndio walikuwa wa kwanza kutoka nje wakiwa wameshika bendera ya taifa na kulakiwa na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania TFF, viongozi wa serikali wakiongozwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda pamoja na mashabiki.
Ilipotimia saa 3:30 msafara wa timu hiyo ulianza safari kuelekea katika Hoteli ya Kilimanjaro Kempinski ilipoandaliwa hafla fupi ya kuwapongeza na ulifika nje ya uzio wa uwanja, mamia ya mashabiki waliojitokeza walilipuka kwa shangwe, lakini msichana mmoja aliyekuwa akiongoza shughuli hiyo pale uwanjani aliamuru msafara huo urudi ndani kwani Waziri Mkuu Pinda alitarajiwa kuwasili kwa ajili ya kuwapongeza wachezaji.
Msafara wa Waziri Mkuu uliingia uwanjani hapo saa 3:50 na aliposhuka kwenye gari alianza kusalimiana na wachezaji na benchi la ufundi na baada ya kutoa pongezi na salamu kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete aliahidi kutoa Shilingi Milioni 3 kama zawadi yake binafsi kwao.
Baada ya Waziri Mkuu kuondoka, msafara wa timu uliondoka kupitia Barabara ya Nyerere, Mandela, Uhuru, Mtaa wa Msimbazi, Barabara ya Morogoro, Bibi Titi, Azikiwe mpaka hoteli ya Kilimanjaro Kempinski.
Katika barabara na mitaa yote ulipopita msafara huo, mashabiki lukuki wake kwa waume bila kujali jua kali lililokuwa likiwaka muda wote waliongozana na msafara huo na wengine wakiwa wamejipanga barabarani kwa ajili ya kuwapongeza wachezaji ambao nao walionekana kuwa wenye furaha muda wote.
Kivutio walikuwa Haruna Moshi 'Boban', Athumani Idd 'Chuji', Mrisho Ngassa, Nurdin Bakari, Jerry Tegete, Meshack Abel, Shaaban Dihile, Kelvin Yondani, Uhuru Selemani na Godfrey Bonny kutokana na kuteremka kutoka katika gari la wazi waliloandaliwa na kuanza kucheza muziki uliokuwa ukipigwa kutoka kwenye gari hilo.
Wakazi wa jiji nao waliziacha shughuli zao na kujitokeza kwa wingi kuwalaki mashujaa hao na kusababisha msongamano mkubwa wa magari.
Kocha wa timu hiyo, Mbrazili Marcio Maximo aliwapongeza wachezaji wake kwa kujituma na kupata ushindi huo na kuongeza kuwa sasa soka ya Tanzania inaanza kusimama na kuahidi kuwa wanakwenda Ivory Coast kushindana na si kushiriki.
Kabla ya kuitoa Sudan, Stars iliitoa Kenya kwa mabao 2-1, ikaisambaratisha Uganda mabao 3-1. Sasa, inasubiri fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) zilizopangwa kufanyika Ivory Coast Februari mwakani.
Mara ya mwisho Stars kufuzu kwa fainali za Afrika ilikuwa mwaka 1980 zilizofanyika nchini Nigeria.
No comments:
Post a Comment