Wednesday, December 24, 2008

Wanajeshi wachukua nchi Guinea

Taarifa ya jeshi la Guinea imesema serikali imevunjwa baada ya kifo cha rais Lansana Conte.

Afisa mmoja wa kijeshi amesema kupitia redio ya taifa kuwa kutakuwa na baraza la utawala litakalohusisha raia na wanajeshi.

Umoja wa Ulaya umelaani hatua hiyo.

Inasemekana mjini Conakry mizinga imeonekana ikiranda katika mitaa ya mji huo.

Lakini waziri mkuu wa Guinea Ahmed Tidiane Souare amesema serikali haijavunjwa na kuwa 'inaendelea kufanya kazi kama kawaida'.

uasi

Spika wa bunge la nchi hiyo Aboubacar Soumpare, ambaye ni mrithi wa rais kwa mujibu wa katiba, ameiambia televisheni moja ya Ufaransa kuwa kuna jaribio la uasi, lakini hadhani kama wanajeshi wote wanaunga mkono hatua hiyo.

Spika huyo awali alitangaza kifo cha rais Conte aliyetawala taifa hilo la Magharibi mwa Afrika kwa miaka 24.

Alisema alifariki kutokana na 'ugonjwa wa muda mrefu'.

Siku 40 za maombolezo zimetangazwa.

Sababu ya kifo cha rais huyo bado haijajulikana lakini rais Conte mwenye umri wa miaka 74 alikuwa mvutaji sigara na kusumbuliwa na maradhi ya kisukari na vilevile inaaminiwa alikuwa na saratani ya damu.


Source: BBC

No comments:

Post a Comment