Tuesday, December 9, 2008

Ramos bosi mpya Real Madrid

Real Madrid wamemchagua kocha wa zamani wa Tottenham Juande Ramos kuwa kocha wao mpya kwa mkataba wa miezi sita baada ya Bernd Schuster kufungishwa virago vyake.

Bernd Schuster alikuwa hana uhakika na kazi yake baada matokeo mabovu msimu huu.Timu hiyo ipo pointi tisa nyuma ya wapinzani wao wa jadi Barcelona.

Madrid itakutana na mahasimu wao hao jumamosi ijayo Nou Camp.

Bodi ya Madrid ambayo ilikuwa ikimkingia kifua Schuster iliamua kumfukuza baada ya Madrid kutandikwa na Sevilla 4-3 katika Primera Liga jumapili.

Ramos ataiongoza timu hiyo hadi mwisho mwa msimu huu kwa kuanzia na mechi ya jumatano ya kombe la mabingwa wa ulaya dhidi ya Zenit St Petersburg.

Ramos alikuwa hana kazi tangia Oktoba mwaka huu alipoachia ngazi Tottenham Hotspur ya Uingereza kutokana na matokeo mabaya sana katika historia ya Tottenham Hotspur.

Schuster alianza vizuri mwaka wake wa kwanza Bernabeu, kwa kulibakisha taji la Primera Liga liloletwa mwaka 2007 na kocha aliyemtangulia Fabio Capello.Lakini harakati zake la kulibakisha taji hilo kwa mwaka wa tatu mfululizo zinaelekea kugonga mwamba kutokana na timu kufanya vibaya.

Madrid ambayo kwa sasa inasumbuliwa na tatizo la kuwa na majeruhi wengi ilipata pigo jingine jana baada ya kugundulika mchezaji wa kimataifa wa Mali Mahamadou Diarra atakuwa nje ya uwanja kati ya miezi sita hadi tisa baada ya kuumia goti.

Diarra anaungana na Ruud van Nistelrooy, Gabriel Heinze, Pepe, Wesley Sneijder, Miguel Torres na Ruben katika benchi la majeruhi.

Golikipa wa Madrid Iker Casillas aliwavunja moyo washabiki wa Madrid jumanne, baada ya kusema kuwa Madrid msimu huu haina uwezo wa kutosha kunyakua taji la Primera Liga.

No comments:

Post a Comment