Tuesday, December 9, 2008

Biashara ya kubadili fedha iko juu


WAFANYABIASHARA ya kubadilisha fedha katika maduka ya fedha nchini, wameanza kunufaika baada ya biashara hiyo kuongezeka kutokana na Watanzania wengi kulipia ada za shule kwa watoto wanaosoma nje ya nchi na gharama za matibabu nje, imeelezwa.

Kwa mujibu wa Jarida la kila mwezi la hali ya uchumi wa Tanzania la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) la Agosti mwaka huu, mauzo na manunuzi ya fedha za kigeni yalifikia dola za Marekani milioni 91.2 (zaidi ya Sh bilioni 92) kwa mwezi.

Taarifa hiyo ilisema mauzo yalikuwa Sh bilioni 46 na manunuzi yalifikia Sh bilioni 46 huku manunuzi yakitokana kwa kiasi kikubwa na malipo kwenye elimu na afya na mauzo yakitokana na mapato kutokana na bidhaa zinazouzwa nje.

Watanzania wanaotaka kulipia matibabu au ada za watoto wao wanaosoma nchi za nje hulazimika kubadilisha shilingi za Tanzania kwenda kwenye fedha za kigeni ndipo walipie gharama hizo.

Taarifa hiyo pia imeonyesha ongezeko la mauzo nje ya nchi kwa kipindi hicho hadi Sh trilioni 3.9 ukilinganisha na trilioni 3.5 Agosti mwaka jana.

Mauzo hayo yalikuwa mengi ni kutokana na utalii na dhahabu ikiwa ni asilimia 28 na 21 kila moja.

Dhahabu iliendelea kuongoza miongoni mwa mauzo ya bidhaa zinazouzwa nje ikichukua asilimia 37.4 ya jumla ya mauzo ya bidhaa zisizo za viwandani na bidhaa za viwandani zilikuwa asilimia 17.6 tu.

Ongezeko pia lilionekana kwenye sekta ya usafirishaji ambapo mapato yalipanda kutoka Sh bilioni 312.2 hadi 358.4 kutokana na kuongezeka kwa biashara za usafirishaji bidhaa katika nchi jirani zinazotumia bandari na barabara za Tanzania.

Bidhaa zilizopitia ardhi ya Tanzania ziliongezeka kutoka tani milioni 2.3 hadi milioni 2.6. Katika bei za bidhaa katika soko la dunia, BoT imesema kahawa ya Robusta na Arabica zilionyesha kuongezeka kidogo kwa dola 2.5 na 3.3 kila moja kwa kilo.

Karafuu na Pamba nazo zilipanda kwa dola 4,600 kwa tani na dola 1.7 kwa kila kilo moja. Bei ya katani haikubadilika, lakini dhahabu iliongezeka kwa asilimia 5.7 hadi dola 939.8 kwa aunsi moja kutokana kuporomoka kwa masoko ya fedha nchini Marekani.

No comments:

Post a Comment