Tuesday, December 2, 2008

Wanaokula fedha za Ukimwi kukiona

TANZANIA imeungana na nchi nyingine duniani katika kuadhimisha ' Siku ya Ukimwi, huku kasi ya maambukizo ya virusi vinavyosababisha upungufu wa kinga mwilini(VVU/UKIMWI) ikipungua.

Aidha Serikali imesema kuwa itawachukulia hatua za kisheria na kinidhamu viongozi wa serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali watakaotumia fedha za miradi ya kupambana na ukimwi tofauti na maelekezo ya pesa hizo.

Makamu wa Raisi, Dk.Ali Mohamed Shein alitoa kauli hiyo mjini kigoma jana alipokuwa akilihutubia taifa wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani ambayo ilifanyika kitaifa mkoani humo.

Dk.Shein alisema kuwa zipo taarifa za kufujwa na kutumiwa vibaya kwa fedha za miradi ya kupambana na ukimwi nchini na kwamba kuanzia sasa serikali haitakaa kimya na itachukua hatua madhubuti kuhakikisha kwamba wale wote waliohusika na matumizi mabaya ya fedha hizo wanawajibishwa.

Aliongeza kuwa fedha hizo zinozotolewa na serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo duniani zinalengo la kuhakikisha kuwa mkakati uliowekwa wa kupunguza maambukizi mapya na kuhudumia wale walioathirika unatekelezwa na kupata mafanikio.

Sambamba na hilo Makamu wa Raisi alisema kuwa serikali itawachukulia hatua viongozi wa serikali watakaoshindwa kuwajibika katika kusimamia utekelezaji wa mipango ya kupambana na ukimwi.

Alisema kuwa kauli mbiu ya mwaka huu inatoa changamoto kubwa kwa Wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa Halmashauri kusimamia vyema mkakati huo wa kupambana na ukimwi na kuondoa mambukizi mapya.

Alibainisha kuwa kila kiongozi mahali pake pa kazi anapaswa kutambua na kutekeleza jukumu la kupambana na ugonjwa huo na kuwa mfano kwa wale walio chini yake.

Dk.Shein pia alizitaka halmashauri za wilaya,miji na jiji nchini kusimamia vyema matumizi ya fedha za kupambana na ukimwi katika maeneo yao na kutoa taarifa kwa wakati kwa ofisi ya Waziri Mkuu tawala za mikoa na serikali za mitaa mara mbili kwa mwaka.

Alieleza kuwa serikali imeshatoa agizo kwa makatibu wakuu wa wizara wakuu wa taasisi wa mashirika ya serikali, mashirika yasiyo ya serikali na idara mbalimbali kutengeza mipango ya kudhibiti ukimwi katika maeneo yao.

Akizungumzia kuongezeka kwa maambukizi mapya nchini alisema kuwa takwimu zinaonyesha kupungua kwa maambukizi mapya kutoka asilimia saba mwaka 2005 na kufikia asilimia 5.8 mwaka jana lakini hiyo bado haitoshi.

Dk.Shein alisema kuwa bado wananchi hawajaweza kubadili tabia za mienendo yao ya kuondokana na maambukizi mapya licha ya kupata elimu na habari kuhusu hali ya maambukizi nba amevitaja vitendo vya zinaa, matumizi ya madawa ya kulevya na mila potofu kwamba bado vinaongoza katika kuchangia maambukizi nchini.

Alisema kuwa msingi mkubwa ni kwa wananchi wenyewe kubadili mienendo ya tabia zao na kuachana na mambo ambayo yatachangia katika kuongezeka kwa maambukizi na hilo lipo ndani ya uwezo wa wanajamii wenyewe.

Awali Waziri wa afya Dk.David Mwakyusa alisema kuwa vituo 300 vya upimaji wa virusi vya ukimwi na ushauri nasaha vimejengwa nchini na kwamba vituo vingine 400 vinatarajiwa kufunguliwa katika zahanati mbalimbali.

Alisema kuwa kuongezeka kwa ujenbzi wa vituo hivyo vya ushauri nasaha na upimaji wa virus vya ukimwi unatokana na kuwpo kwa mwitikio mzuri wa wananchi katika kujitokeza kupima afya zao kwa hiari.

Naye Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi, Dk.Fatma Mrisho alisema kuwa bila kushirikishwa kwa wanaume katika kupambana na ugonjwa huo itakuwa vigumu kupata mafanikio ya kudhibiti maambukizi mapya.

Alisema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa wanawake ndiyo walioathjirika kwa wingi na kwa sababu ndiyo waliojotokeza kwa wingi kupima afya zao lakini wanaume ni lazima wahamaishwe na kushirikishwa kwa karibu ili kuzuia.

Dk.Mrisho alikiri kuwepo kwa changamoto za kukabiliana na kudhibiti maambukizi mapya na kusema kwamba ni lazima kamati mbalimbali zihusishwe kwa karibu katika utekelezaji wa mkakati wa kupambana na ugonjwa huo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Abbas Kandoro ameziagiza halmashauri mkoani kusimamia utekelezaji wa mpango wa kila familia kuhusika katika malezi ya yatima katika vituo na majumbani mwao.

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Fabian Massawe katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliofanyika kimkoa katika Kata ya Manzese, Wilaya ya Kinondoni, Kandoro amesema kila halmashauri inahusika katika kuzingatia na kusimamia utekelezaji wa mpango wa kila familia kulea yatima angalau mmoja.

Alisema watoto yatima wanahitaji upendo kama wengine.

Alisema watoto hao wamekuwa wakikosa upendo na faraja ya famili kwa kutokana na vifo vya wazazi wao ambao wengi wao wamekufa kwa ugonjwa wa Ukimwi hivyo ni jukumu la jamii kuwalea watoto hao.

“Jamii ihusike kulea watoto yatima, naagiza halmashauri zote mkoani hapa ziangalie utaratibu unaofaa na kusimamia malezi ya watoto kupitia kila familia, yaani kila familia ihusike kulea yatima,”

No comments:

Post a Comment