Wednesday, December 24, 2008

Simba yafungasha virago

Simba jana ilitupwa nje ya michuano ya soka ya Kombe la Tusker baada ya kulazwa na URA ya Uganda 2-1 katika mchezo wa nusu fainali ya michuano hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa, jijini, Dar es Salaam.

Kwa matokeo hayo sasa, URA, itakuwa inasubiri mshindi wa mechi ya leo kati ya Mtibwa na Tusker ili kukabiliana naye kwenye fainali, ambapo Simba itacheza mechi ya kusaka nafasi ya tatu.

Mara baada ya mpira kumalizika mashabiki wa Yanga walianza kuimba kwa nguvu wimbo maarufu wa `parapanda inalia`.

Hata hivyo, Simba ilipoteza mchezo huo kutokana na makosa ya kizembe ya mabeki wake waliokuwa wakiacha mpira na kuwahiwa na washambuliaji wa URA.

Pia itajutia nafasi kadhaa za wazi ilizokosa kutokana na ubutu wa safu yake ya ushambualiji.

Simba, hata hivyo, ndio ilianza kwa kishindo mchezo huo na kujipatia bao la kwanza lililofungwa katika dakika ya nne na Henry Joseph baada ya kuunganisha krosi ya Ulimboka Mwakingwe.

Bao hili lilionekana wazi kuizindua URA na kupeleka mashambulizi makali langoni mwa Simba na kujipatia bao katika dakika ya 44.

URA iliweza kusawazisha kwa bao lililopachikwa na Tonny Maweje, ambaye aliwahi mpira ulioachwa na Ramadhan Wasso.

Waganda hao walikianza kipindi cha pili kwa nguvu na kuweza kujipatia bao la pili lililofungwa na Eric Obua baada ya kupokea pasi ya Ismail Kigozi, ambaye aliwahi mpira uliokuwa umeachwa na mabeki wa Simba waliodhani kuwa unatoka nje.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Kocha Mkuu wa Simba, Talib Hilal alieleza kuwa timu yake haikuwa makini katika kujihami.

Talib alidai timu yake baada ya kupata bao la kuongoza ilijisahau na kuanza kushambulia bila ya kujihami vizuri.

Alieleza kuwa timu yake ilipoteza umakini, ambapo pasi zao nyingi zilikuwa zinanaswa na wapinzani wao.

Kocha wa URA, Moses Basena alisema timu ilistahili kushinda kutokana na kucheza soka ya juu.

Basena alisema, hata hivyo, iliathiriwa na joto kutokana na mchezo huo kuanza saa tisa na nusu alasiri.

Simba: Deo Bonaventura, Salum Kanoni, Ramadhan Wasso, Meshack Abel, Kelvin Yondani, Henry Joseph (Nico Nyagawa dk.58), Haruna Moshi `Boban`, Mohamed Banka
(Obinna Orji dk.71), Mussa Hassan `Mgosi`, Emeh Ikechukwu na Ulimboka Mwakingwe (Ramadhan Chombo dk.60).

URA: Dhairi Abel, Sam Mubiru, David Kyobe, Joseph Owino, John Karangwa, Marco Kawemba, Tonny Mawejje (Kaira Phiri dk.92), Patrick Ochan, Ismail Kigozi, Maritin Muwanga(Henry Kisseka dk.84) na Eric Obua (Osama Farouk dk.67).

Wakati huo huo, Mtibwa inaivaa Tusker ya Kenya leo katika nusu fainali nyingine ya michuano hiyo itakayochezwa Uwanja wa Taifa, jijini, Dar es Salaam.
Mshindi kati ya timu hizo mbili ndio ataivaa URA katika fainali ya mashindano hayo.



Source: Nipashe

No comments:

Post a Comment