Tuesday, December 30, 2008

Obinna asimamishwa Simba

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Simba kutoka Nigeria, Orji Obinna, amezusha tafrani nyingine katika timu hiyo na uongozi wa klabu hiyo umemsimamisha kwa muda usiojulikana.

Mbali ya kusimamishwa kwa mchezaji huyo, uongozi wa Simba umemtimua kambini mchezaji Emmanuel Gabriel.

Katibu Mwenezi wa Klabu hiyo, Said Rubeya, alisema jana kuwa Obinna amesimamishwa na Kamati ya Utendaji kutokana na utovu wa nidhamu.

Rubeya alisema Kamati ya Utendaji ilifanya mkutano wake juzi na kuamua kumsimamisha mchezaji huyo kutokana na utovu wa nidhamu uliokithiri, na kumpiga marufuku Gabriel kuendelea kukaa katika kambi ya timu hiyo kwa alichosema mchezaji huyo kukiuka taratibu za kujiunga na timu ya Fanja FC ya Oman alikouzwa.

Alisema kikao hicho kilitoa maazimio hayo baada ya kuona Kamati ya Nidhamu iko kimya licha ya wachezaji hao kwenda kinyume na taratibu za klabu hiyo.

Alisema Obinna amekuwa akionywa mara kwa mara kutokana na vitendo vyake mbalimbali vinavyoharibu sifa ya timu, pamoja na kuwaudhi wachezaji wenzake.

Alisema Mnigeria huyo licha ya kuonywa kwa vitendo vya ulevi, kutokaa kambini, amekuwa akiwadharau viongozi wake na kutotii maelekezo anayopewa, hali ambayo imeifanya kamati hiyo kumsimamisha.

Alisema kikao hicho pia kilirejea matendo kadhaa ya mchezaji huyo ikiwemo kitendo cha kumpiga aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Krasmir Bezinski, pamoja na kutoroka kambini na kwenda kunywa pombe katika kumbi za starehe.

Mchezaji huyo pamoja na Mnigeria mwenzake, Emeh Izechukwu, waliwahi kusimamishwa na timu hiyo mwishoni mwa mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ya Tanzania Bara, na walisamehewa na kurejea kundini hivi karibuni.

Akimzungumzia Gabriel, Rubeya alisema licha ya mchezaji huyo kuuzwa kwa timu ya Fanja, bado ameendelea kuwepo ndani ya kambi ya timu hiyo hali ambayo ni kinyume cha taratibu.

Alisema Gabriel kwa sasa ni mali ya timu hiyo ya Oman, hivyo anatakiwa kufuata taratibu za Fanja na si Simba tena, kwa kuwa si mchezaji wao halali.

Rubeya alisema uongozi wa klabu yake umeliandikia barua Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kuijulisha hali hiyo.

No comments:

Post a Comment