Saturday, December 13, 2008

MWANAFUNZI MTANZANIA AKAMATWA NA DAWA ZA KULEVYA INDIA

WATANZANIA watatu akiwamo mwanafunzi, wanashikiliwa na polisi nchini India kwa tuhuma za kukutwa na kilogramu 20 za dawa za kulevya.

Tukio hilo linaloelezwa na polisi kuwa la kwanza kuwahusisha Watanzania nchini India, lilitokea Jumatano iliyopita katika mji wa Basni jijini Jodhpur.

Msemaji wa polisi wa jiji hilo Girraj Meena, alisema Watanzania hao walikamatwa na dawa za kulevya aina ya Heroin mara baada ya kuzipokea kutoka kwa watu ambao mpaka sasa, polisi haijawakamata.

Alisema kinara wa Watanzania hao ni Adam Godwin (41), mwenye visa ya biashara nchini humo ambaye amekuwa akitafutwa kwa tuhuma za kuhusika na biashara ya dawa za kulevya kwa miaka kadhaa sasa.

"Godwin amekuwa akija India mara nyingi na kabla ya kufika hapa (India) amewahi kutembelea China, Macao, Hong Kong na Nepali," alisema Kamanda huyo na kubainisha kuwa mtuhumiwa huyo ana uhusiano wa karibu na mtuhumiwa wa Kimataifa wa dawa za kulevya kutoka barani Afrika mwenye mtandao mkubwa katika nchi za Tanzania, Uganda, na Kenya, Abu Baquar.

Kamanda Meena aliwataja Watanzania wengine waliokamatwa katika tukio hilo kuwa ni mwanafunzi wa kompyuta katika moja ya vyuo vilivyoko mjini Mumbai Adam Mohammad (32) and Umar Yousuf (25). Yousuf amekuwa akiishi mjini New Delhi tangu miezi miwili iliyopita.


"Polisi waliwakamata watuhumiwa hao walipokuwa wakijiandaa kuondoka kuelekea Jaipur mara baada ya kupokea mzigo huo baada ya kupata taarifa za awali," alisema Meena.

Akifafanua alisema dawa hizo zilifungwa katika mifuko 20 yenye uzito wa kilogramu moja kila moja. Alisema "Dawa zinasadikika kutoka nchini Pakistan na zilikuwa zikisafirishwa kwenda barani Afrika kupitia miji ya Jaipur na Delhi.

Miji ya Jaipur na Delhi ndiyo inayotumika na wafanyabiashara wengi kusafirisha dawa za kulevya kutoka nchi za Pakistan, Afghanistan na maeneo mengine ya dunia kuja Afrika.

Meena alisema, mbali na Watanzania hao kukamatwa na dawa hizo, pia walikutwa na fedha za nchi mbalimbali ikiwamo dola 3000 za Marekani na Rupia 13,080 za India. 

Kwa mujibu wa Meena Watanzania hao walifika mjini Basni siku mbili kabla ya kupokea mzigo huo na walikamatwa walipokuwa wakijiandaa kuondoka.

"Uchunguzi wa awali wa kipolisi umeonyesha kuwa Watanzania hao ni madalali waliokuwa wakikusanya mzigo huo ambao wangeusafirisha kwa wafanyabiashara wa Afrika," alisema Meena na kueleza kuwa tayari polisi imefungua kesi kuhusu tukio hilo.

Taarifa hizo za kipolisi zimeeleza kuwa dawa walizokamatwa nazo Watanzania hao ni za daraja la kwanza katika ubora na mara nyingi huuzwa kwa gharama kubwa duniani kote.

No comments:

Post a Comment