Tuesday, December 23, 2008

Ivo aitwa K`njaro Stars

Kocha mkuu wa timu ya soka ya taifa, Marcio Maximo amemuita kipa wa zamani wa klabu ya Yanga, Ivo Mapunda katika kikosi cha timu ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars kitakachoshiriki katika mashindano ya Kombe la Chalenji yanayotarajiwa kuanza kufanyika Desemba 31, jijini, Kampala, Uganda.

Ivo ambaye alikuwa ni kipa namba moja wa Stars tangu kuwasili kwa Maximo alishindwa kuidakia timu hiyo ilipokuwa inacheza na timu ya taifa ya Sudan hivi karibuni kutokana na kusajiliwa na klabu ya St. George ya Ethiopia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa Shirikisho la soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye, Tanzania Bara ni moja kati ya nchi nne zilizowasilisha majina ya wachezaji wake itakaowatumia katika mashindano hayo ya mwaka huu.

Musonye aliwataja wachezaji wengine ambao wataichezea timu ya Bara maarufu kwa jina la Kilimanjaro Stars kuwa ni pamoja na Shabani Dihile, Shadrack Nsajigwa, Nurdin Bakari, Kevin Yondani, Salum Swedi, Meshack Abel, Juma Jabu, Amir Maftah na Henry Joseph.

Wengine ni Geofrey Bonny, Athuman Iddi `Chuji`, Shabani Nditi, Haruna Moshi `Boban`, Nizar Khalfan, Kigi Makasi, Uhuru Selemani, Mrisho Ngassa, Mussa Hassan `Mgosi` na Jerryson Tegete.

Musonye alisema kuwa nchi nyingine zilizowasilisha majina ya wachezaji wake ni pamoja Sudan, Zambia na Burundi.

Aliongeza kuwa maandalizi ya mashindano hayo yamekamilika na Rais wa CECAFA, Leodegar Tenga alikuwa Kampala hivi karibuni kukagua viwanja vitakavyotumika katika mashindano hayo.



Source: Nipashe

No comments:

Post a Comment