Saturday, December 20, 2008

RAIS KIKWETE AWASHUTUMU WATENDAJI ATCL KWA UZEMBE

WAKATI Rais Jakaya Kikwete amesema kuwa kufungiwa kwa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), kumetokana na uzembe wa watendaji wa shirika hilo, Waziri wa Miundombinu, Shukuru Kawambwa ameipa bodi ya shirika hilo siku saba kueleza chanzo cha kudorora kwake. ATCL imefungiwa kurusha ndege zake ndani na nje ya nchi baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Anga (TCAA), kuipokonya cheti cha usalama wa anga (AOB) kutokana na uzembe katika kujaza nyaraka za usalama wa anga kulingana na sheria za mamlaka hiyo.

Hatua ya TCAA ilifuatiwa na uamuzi wa Umoja wa Mashirika ya Ndege Duniani (IATA) kuizuia kufanya shughuli zozote za biashara ya usafiri wa anga.

Kikwete, ambaye yuko nchini Msumbiji kwa ziara ya siku tatu ya kikazi, alisema katika utaratibu wa kawaida shirika hilo na mengine hufanyiwa ukaguzi na TCAA na kwamba, katika kipindi hicho ATCL ilipewa notisi ya miezi mitatu na muda wa ziada kuwasilisha nyaraka zake kwa ukaguzi.

Lakini akaongeza kuwa pamoja na kuongezewa muda, shirika hilo lilishindwa kufanya hivyo na badala yake ATCL ikawasilisha TCAA nyaraka zenye mapungufu na kusababisha kufungiwa.

Rais Kikwete aliyekaririwa na kituo cha televisheni cha TBC1 kutoka Msumbiji juzi usiku na jana, amemtaka Waziri wa Miundombinu kukutana na bodi ya ATCL haraka, kuhakikisha bodi hiyo na menejimenti inatoa maelezo kuhusu uzembe huo pamoja na kuchukua hatua kuiwezesha ATCL kuanza kazi ndani ya siku 10.

Kwa mujibu wa TBC1, sambamba na hatua hiyo, serikali pia ipo mbioni kuiongezea mtaji ATCL kwa lengo la kuiwezesha kuboresha huduma zake na kujiendesha kibiashara.

Katika miezi ya karibuni ATCL imekumbwa na wimbi la matatizo mbalimbali, ikiwemo hali mbaya kifedha iliyosababisha wafanyakazi wake kulipwa kwa mafungu mshahara wao wa mwezi Novemba.

Hata hivyo, bodi ya ATCL imesisitiza kuwa serikali isipolipa deni la Sh20 bilioni na kuongeza mtaji wa Sh70 bilioni, itakuwa ndoto kufanikisha mipango ya kuliunda upya shirika hilo, anaripoti Leon Bahati.

Mwenyekiti wa bodi hiyo, Balozi Mustapha Nyang’anyi alisema dawa ya ATCL ni kulipa deni hilo na kuongeza mtaji kwa dola 67 milioni za Kimarekani.

Alikanusha madai kuwa kuyumba kwa ATCL kumetokana na uzembe wa watendaji, akisema tatizo kuu ni serikali kutotekeleza ahadi za kulifufua shirika mara baada ya kuvunja mkataba na Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) Machi, 2007.

“Hata tukirudishiwa leseni bado hatuwezi kutatua matatizo hayo. Kama serikali ingelipa deni, angalau tungeweza kukopa benki. Lakini katika mazingira ya deni hili hatuwezi kukopeshwa,” alisema waziri huyo wa zamani wa mawasiliano na uchukuzi.

“Udhaifu wote unaoonekana sasa tuliuona tangu awali na ndio maana tuliiambia serikali watupe fedha hizo za kulisuka upya shirika. Uzuri, wao (serikali) ndio waliotuomba tufanye tathmini na Aprili 30 mwaka 2007 tukaikabidhi Wizara ya Miundombinu mpango wa biashara wa miaka mitano pamoja na kiwango cha fedha kinachohitajika. Hadi leo hatujapewa chochote,” alilalamika Balozi Nyang’anyi.

Katika hatua nyingine, serikali imempa siku saba mwenyekiti wa bodi ya ATCL kutoa maelezo ya kina yaliyosababisha shirika hilo kupoteza mwelekeo na kusimamishiwa leseni ya kuruka angani- siku zinazoisha Desemba 22, anaripoti Peter Edson.

Serikali pia imesema ili ATCL iweze kurudishiwa leseni yake na kuanza kufanya kazi kama ilivyokuwa mwanzo ikizingatia taratibu zote za Mamlaka ya anga duniani, inahitaji kiasi cha Dola 273 milioni za Kimarekani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam jana, Waziri wa Miundombinu, Dk. Shukuru Kawambwa alisema serikali imesikitishwa sana na kitendo cha ATCL kusimamishiwa leseni, akisema suala hilo linaathiri uchumi wa nchi.

“Hatuwezi kuoneana aibu mambo ya nchi yanapoharibika, tumempa mwenyekiti wa bodi siku saba kutoa maelezo ya kina, ili waliohusika kuliangamiza shirika waweze kuwajibishwa,” alisema Dk. Kawambwa.

Alisema fedha ambazo zinatakiwa ili kuirudisha ATCL katika shughuli zake za kawaida ni nyingi, ikizingatiwa kuwa hazikuwa kwenye bajeti yoyote ile.

Alisema serikali kwa kushirikiana na bodi ya wakurugenzi tayari imeshazipata fedha hizo na tayari juhudi za kupitia upya kanuni na sheria za uendeshaji wa ndege zimeanza kufanyika ili kulinusuru shirika hilo.

Dk. Kawambwa alisema utekelezaji wa mpango huo wa kuboresha shughuli za shirika, kwa lengo la kukidhi kanuni na sheria stahili za mamlaka ya anga ulishaanza tangu Desemba 11 na unategemewa kuisha Desemba 24 wakati ndege za ATCL zitakaporejea angani.

Aliongeza kuwa mkurugenzi huyo akishapeleka maelezo ya kina kuhusu sakata hilo, watendaji wote watakaobainika kuwa kwa namna moja au nyingine walihusika kulihujumu shirika hilo watawajibishwa kwa kanuni na sheria.

“Katika jambo hili hatuna masihara hata kidogo, tutahakikisha tunapata ufafanuzi wa kutosha na kuchukua hatua kwa masilahi ya taifa,” alisema Dk. Kawambwa

Alisema haitawezekana watu wachache kuharibu kazi na uchumi wa taifa wakati serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya kuliboresha shirika hilo ili liweze kumudu shughuli zake.

Alisema kusimamishwa kwa ATCL kuruka angani ni changamoto kwa nchi, kwani athari zake ni kubwa kutokana na ukweli kuwa litakuwa haliingizi fedha yoyote.

“Watumishi wa ATCL wataendelea kudai mishahara yao kwa mujibu wa taratibu, lakini shirika halizalishi, fedha za mishahara zitatoka wapi?” Dk. Kawambwa alihoji.

Alisema pamoja na changamoto hiyo, bodi ya wakurugenzi pamoja na shirika hilo wanawajibika kutafuta fedha za mishahara ya wafanyakazi wao katika kipindi hiki ambacho huduma zimesitishwa.

“Tumewaeleza kuwa serikali haitapenda kusikia wafanyakazi wanakosa mishahara “

Alisema nia ya serikali ni kuhakikisha kuwa ATCL inarudia kazi zake mapema iwezekanavyo na kwa ufanisi, ikiwa ni pamoja na kuleta maendeleo ya taifa badala ya kuwanufaisha watu wachache.

Hatua ya TCAA kuipokonya cheti cha usalama wa anga ilichukuliwa baada ya Kitengo cha Ukaguzi cha Umoja wa Mashirika ya Ndege Duniani (IOSA) kulikagua shirika hilo mwaka jana na kubaini mapungufu 482, lakini ATCL haikurekebisha makosa hayo.

Novemba mwaka huu, Mamlaka ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga (ICAO) iliikagua TCAA na kubaini kuwa nyaraka zilizojazwa na ATCL zilikuwa haziendani na sheria za mamlaka hiyo ya Tanzania na hivyo kuishauri iipokonye cheti hicho cha usafiri wa anga.

Tayari ATCL imeshasema kuwa imerekebisha mapungufu hayo na kuziwasilisha nyaraka hizo TCAA, ambayo iliahidi kuzishughulikia katika muda wa siku 10 za kikazi.

Mwandishi wetu, Salim Said anaripoti kuwa baadhi ya Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, ambazo ni kati ya waathirika wa matatizo ya usafiri ya ATCL, zimepongeza uamuzi wa IATA wa kulifungia shirika hilo la ndege.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam jana, makatibu Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) na Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu wamesema hatua hiyo ni stahili ya ATCL na wala si uonevu.

Katibu mkuu wa Bakwata, Sheikh Ally Juma Mzee alisema kutokana na utendaji mbovu wa ATCL, Waislamu 1,500 walipata usumbufu wa kulala Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere kwa zaidi ya siku 11 mwaka jana wakati wakielekea Maka kwenye ibada ya Hija.

Licha ya Usumbufu huo lakini Waislamu/mahujaji hao hawakulipwa fidia pamoja na serikali kuwaahidi kifuta jasho, jambo lililozipelekea baadhi ya Taasisi za Kiislamu kuingilia kati na kuahidi kuwa wataliburuza mahakamani shirika hilo.

“Waislamu nchini ndio waathirika wakuu wa uzembe wa viongozi wa ATCL, hatua ya kuifungia si uonevu bali ni stahili yao kutokana na uzembe unaofanywa na uongozi wa shirika hilo,” alisema Sheikh Mzee.

“Hili ni fundisho kwanza kwa uongozi wa ATCL na ni aibu kwa shirika linaloongozwa na wasomi na watu ambao walishashika nafasi kubwa serikalini kufanya uzembe wa hali ya juu katika utendaji wao,” alisema.

Naye katibu mkuu wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislaam Tanzania, Sheikh Ramadhan Sanze alisema hatua hiyo ni sahihi na kulaumu kuwa imechelewa kwa kuwa ilistahili kuchukuliwa tangu mwaka jana wakati shirika hilo lilipokwamisha safari za mahujaji.

“Hii ilikuwa ichukuliwe tangu mwaka jana imechelewa sana, lakini tatizo si ATCL bali tatizo ni viongozi wake ambao ni wazembe na hawana historia nzuri ya utendaji katika sehemu zote wanazoongoza,” alisema Sheikh Sanze.

Sheikh Sanze alisema mwenyekiti wa bodi ya ATCL, Mustapha Nyang’anyi ana kashfa ya kununua kivuko kibovu cha Kigamboni katika miaka ya tisini wakati huo akiwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi.


Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment