Friday, December 19, 2008

Waziri Mkuu wa zamani Ethiopia atoka gerezani

Waziri Mkuu wa zamani wa Ethiopia Tamerat Layne ameachiliwa huru baada ya kutumikia kifungo cha miaka 12 jela kutokana na makosa ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.

Alitimuliwa serikalini mwaka 1996 na miaka minne baadae akatiwa hatiani na mahakama kuu ya Ethiopia.

Alihukumiwa kutumikia miaka 18 jela, lakini ameachiliwa mapema kutokana na kuonesha tabia njema alipokuwa akitumikia kifungo.

Aliwahi kuwa rafiki wa karibu wa Waziri Mkuu wa sasa Minister Meles Zenawi, na muungano wao ndio ulioangusha utawala wa kijeshi mwaka 1991.

Tamerat Layne alikuwa miongoni mwa viongozi wakuu watatu wa muungano wa chama cha demokrasia na kimapinduzi wa Ethiopia.

Mwengine alikuwa Seye Abreha, aliyewahi kuwa waziri wa ulinzi, lakini pia akafungwa pamoja na Tamerat kutokana na makosa kama hayo ya rushwa.

Seye aliachiliwa huru mwaka jana

Hata hivyo inasemekana, ingawa wananchi wa Ethiopia hawapingi tuhuma hizo za rushwa dhidi ya watu hao wawili, lakini pia wanadhani suala la kupigania madaraka ndani ya chama hicho nalo lilichangia kufungwa watu hao.

No comments:

Post a Comment