Tanzania kwa mara ya mwisho ilifuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 1980 ikiwa ni takribani miaka 28 iliyopita.
Stars, imefuzu kwa fainali hizo za Mataifa ya Afrika zinazoshirikisha wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani, baada ya kuifungisha virago Sudan kwa jumla ya mabao 5-2 kufuatia ushindi wa 3-1 wa Stars iliyoupata katika mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita.
Hii ni mara ya pili kwa Tanzania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika, ambapo kwa mara ya kwanza ilishiriki mwaka 1980 fainali hizo zilipochezwa Nigeria.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera ambaye jana alikuwepo uwanjani kushuhudia, mwaka 1980 alikuwa kocha wa Stars iliyoshiriki fainali hizo za Afrika.
Stars iliandika bao la kuongoza katika dakika ya tisa lililowekwa kimiani na Henry Joseph baada ya kazi kubwa iyofanywa na Mrisho Ngasa aliyeinyanyasa ngome ya Wasudan na kutoa pande kwa mfungaji aliyeukwamisha wavuni.
Hata hivyo, mchezo wa kujihami wa Stars, ulisababisha Sudan kupata bao la kusawazisha katika dakika ya 45 na hivyo kuwaweka roho juu waTanzania waliokuwa wakisubiri kwa hamu ushindi wa timu yao.
Timu ya taifa ya Tanzania ilipata bao la pili katikati ya kipindi cha pili lililofungwa na Nurdin Bakari, na kuihakikishia timu hiyo nafasi ya kwenda Ivory Coast mwakani kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani tu.
Stars katika mbio zake za kusaka nafasi ya kwenda Ivory Coast ilifungwa 1-0 na Kenya huko Nairobi Machi 29 kabla ya kuifunga Harambee Stars kwa bao 2-0 Aprili 12 jijini Dar es Salaam, na kuibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Uganda katika mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Mei 3 na kutoka sare ya 1-1 katika mchezo wa marudiano uliofanyika Kampala Mei 17 mwaka huu.
Ofisa Habari wa TFF, Shirikisho la Soka Tanzania, Florian Kaijage alisema kwa njia ya simu kuwa kocha wa Stars, Mbrazil Marcio Maximo alisema kuwa mchezo ulikuwa mgumu kama alivyotarajia, lakini anachoshukuru ni kwa wachezaji wake kufuata maelekezo na kupata bao la mapema lililowachanganya Sudan.
``Nilijua Sudan wakiwa kwao watashambulia sana na mchezo utakuwa mgumu, lakini niliwaambia vijana wangu na ninachoshukuru walifuata maelekezo na kupata bao la mapema lililowachanganya Sudan, tunashukuru tumefuzu kwenda Ivory Coast, ``Kaijage alimkariri Maximo aliyezungumza baada ya mchezo huo.
Ushindi wa Stars umevunja mwiko wa kutolewa na Sudan katika mashindano mbalimbali ya mtoano baada ya kutolewa mara tatu.
Pia imevunja mwiko wa Sudan kutofungwa kwenye uwanja wa nyumbani kwani mara ya mwisho ilifungwa na Ivory Coast mwaka 2005. Hii ni mechi ya 11 kwa Taifa Stars kushinda tangu ianze kunolewa na Kocha Marcio Maximo.
Timu inatarajia kurejea nchini kesho saa 3 asubuhi kwa ndege ya Kenya Airways.
Kikosi cha Stars kilichoanza:Shaban Dihile, Shadrack Nsajigwa, Juma Jabu, Salum Sued, Nadir Haroub 'Canavaro', Geofrey Bony, Mrisho Ngasa, Henry Joseph, Haruna Moshi, Jerson Tegete na Nurdin Bakari.
No comments:
Post a Comment