Sunday, December 28, 2008

Mtibwa mabingwa wapya wa kombe la Tusker


BAO la mkwaju wa penalti lililopachikwa wavuni na Rashid Gumbo katika dakika ya 60, jana lilitosha kuipa Mtibwa Sugar ubingwa wa kwanza wa Kombe la Tusker tangu kuanzishwa kwake mwaka 2001.

Ikiwa na rekodi ya kufika fainali ya michuano hiyo mara tatu, Mtibwa Sugar ya Manungu - Turiani, Morogoro, jana ilifanya kweli katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa kuwazima URA ya Uganda kwa bao 1-0.

Mechi hiyo iliyokuwa ya ushindani mkubwa kwa dakika zote 90, kipindi cha kwanza, timu zote zilionekana kucheza staili ya kushambulia na kujihami. Katika kipindi cha pili, Mtibwa Sugar walionekana kucheza soka ya kutulia zaidi, lakini URA nayo ikiongozwa na wachezaji kama Tonny Mawejje na Eric Obua, walihaha vilivyo, lakini ngome ya Mtibwa Sugar ikawa imara na kuweza kuokoa michomo ya wapinzani wao.

Katika dakika ya 60, Mtibwa Sugar walifanya shambulizi la nguvu katika lango la URA na katika heka heka hiyo, Idrissa Rajab, akachezewa rafu.

Mwamuzi wa mechi hiyo, Oden Mbaga, akaamuru mkwaju wa penalti ambao ulikwamishwa wavuni kiustadi na Gumbo akimchambua kipa wa URA, Abeid Dhaira. Bao hilo liliongeza kasi ya mchezo huo kwani Mtibwa Sugar walipata nguvu zaidi wakitaka kuongeza huku Wakusanya Kodi wa Uganda, wakipigana vilivyo kusawazisha.

Hata hivyo, ukuta wa Mtibwa Sugar ukiongozwa na Shaaban Nditi, akisaidiwa na Salum Sued, Obadia Mungusa na Chacha Marwa, ulifanya kazi ya ziada kumlinda kipa Shaaban Kado. Hadi filimbi ya mwisho, Mtibwa Sugar, walitoka kifua mbele, hivyo kutwaa ubingwa wa Tusker kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake mwaka 2001.

Simba ndiyo imekuwa kinara kwa kutwaa mara nne huku Kagera Sugar, Yanga na Mtibwa Sugar zikitwaa mara moja kila moja. Safari hii, Simba imeambulia nafasi ya tatu baada ya kuifunga Tusker FC ya Kenya mabao 3-2 katika mechi iliyopigwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Kwa ushindi wa jana, licha ya kuiwezesha Mtibwa Sugar kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza, pia imefanikiwa kulipa kisasi cha kufungwa na URA katika hatua ya makundi. Aidha, kwa ushindi huo, Mtibwa Sugar iliyotokea kundi A, pamoja na timu za Yanga na URA, imejinyakulia kitita cha sh mil. 40, huku URA iliyokamata nafasi ya pili, ikipata sh mil. 20.

Akizungumza baada ya mechi ya jana, Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Salum Mayanga, alisema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuijalia timu yake kufika fainali kwa mara ya tatu na kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza.

Mayanga aliyekuwa na timu hiyo tangu ikiwa Ligi Daraja la Tatu wakati huo akiwa mchezaji, alisema mafanikio hayo ni faraja kubwa kwa benchi la ufundi, wachezaji hadi viongozi wa timu hiyo.

“Namshuru Mwenyezi Mungu kwa mafanikio haya makubwa, kwanza kufika fainali ya michuano hii mara ya tatu, pia kutuwezesha kutwaa ubingwa… haya ni mafanikio makubwa kwetu,” alisema Mayanga. Alisema, mafanikio hayo si fahari kwa Mtibwa Sugar pekee, bali kwa Watanzania wote na anajisikia kuwatendea haki Watanzania wote. “Najisikia kuwatendea haki Watanzania wote,” alisema kocha huyo na kuongeza kuwa anashukuru kwamba, ametimiza ndoto ya kufanya vizuri katika michuano hiyo.

Naye Gumbo, mfungaji wa bao pekee lililopeleka ubingwa katika viunga vya mashamba ya miwa ya Manungu, alisema anajisikia furaha kubwa timu yao kutwaa ubingwa akisema ni juhudi ya wachezaji wote na benchi la ufundi.

Mara ya mwisho Mtibwa Sugar kupata mafanikio makubwa, ilikuwa mwaka 2000, walipotwaa ubingwa wa Bara ukiwa ni wa pili kwani mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 1999. Mtibwa Sugar: Shaaban Kado, Obadia Mungusa, Chacha Marwa, Salum Sued, Shaaban Nditi, Uhuru Selemani, Rashid Gumbo, Abdallah Juma/Yusuph Mgwao, Omar Matuta/Abdulhalim Amour, David Mwantobe/Soud Abdallah.

URA: Abeid Dhaira, Sam Mubiru, David Ryobe, Joseph Owino, John Kangwa/Sadat Kabaire, Manco Kawesa, Tonny Mawejje, Panich Ochan, Ismail Kigozi/Philly Kaira, Martine Mwangwa/Henry Kizacha na Erick Obua.

Baada ya hapo, kilichofuata ni mgeni rasmi katika mechi hiyo, Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk. Diodorus Kamala kukabidhi kombe na kuwavisha medali za dhahabu mabingwa hao.

Mbali ya medali, Mtibwa Sugar wamekabidhiwa mfano wa hundi ya sh mil. 40 huku wachezaji wa URA wakivikwa medali za fedha na kukabidhiwa kombe dogo na mfano wa hundi ya sh mil. 20 huku Simba wakipewa hundi ya sh mil. 10.

Zawadi nyingine zilizotolewa na wadhamini wa michuano hiyo, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), ni Kombe kwa timu yenye nidhamu, ambayo ilikwenda kwa timu ya Simba na kitita cha sh mil. 2.

Aidha, wachezaji Tonny Mawejje wa URA ya Uganda na Mussa Hassan Mgosi, wameibuka kuwa wafungaji bora wa michuano hiyo wakifunga mabao mawili kila mmoja, hivyo kulamba kiasi cha sh mil moja kila mmoja.

Mbali ya wapenzi na mashabiki kushuhudia burudani ya soka, pia walisindikizwa na burudani ya muziki kutoka kwa Tanzania One Theatre (TOT), waliotumbuiza kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mechi hiyo.

Michuano hiyo, ilishindanisha timu sita; ambazo ni Yanga, Simba, Mtibwa Sugar, Prisons, Tusker FC ya Kenya na URA ya Uganda.

No comments:

Post a Comment