Tuesday, December 9, 2008

Rais atahadharisha hali ngumu ya kiuchumi

Rais Jakaya Mrisho Kikwete ametoa tahadhari kuwa hali mbaya ya kiuchumi duniani inaweza kuathiri hali ya uchumi wetu. Akizungumza kwenye baraza la Idi jana Rais Kikwete amewahakikishia wananchi kuwa Serikali yake imejiandaa kukabiliana na hali hiyo. Rais amesema kuwa nchi mbalimbali zilizoendelea zimejikuta katika hali mbaya ya kiuchumi ambayo imesababisha "mamilioni ya watu kupoteza ajira zao". Rais Kikwete pia amehoji kwanini bei ya mafuta nchini haishuki haraka wakati bei hiyo katika soko la dunia imeshuka kwa kiasi kikubwa. "Inashangaza kuwa bei ikipanda kwa haraka kwenye soko la dunia na hapa inapanda kwa kasi sana, lakini sasa imeshuka hapa wamepatwa na kigugumizi" alisema Rais Kikwete. Wakati huo huo, Serikali ya Tanzania imetoa msaada wa madawa, vifaa na nyenzo mbalimbali kuisaidia nchi ya Zimbabwe kupambana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ambao umeshaua zaidi ya watu 500 na ukiendelea kuenea kwa kasi.

Msaada huo umetolewa leo kwa Mwakilishi wa Ubalozi wa Zimbabwe nchini. Afisa wa Wizara ya Afya Bw. Berege amesema kuwa msaada huo umetolewa kwa kuzingatia ushirikiano baina ya nchi zetu mbili.

Vyanzo mbalimbali vinadokeza pia kuwa yawezekana serikali ikaandaa timu ya wataalamu kutoka Tanzania ambao wataenda kushirikiana na wenzao Zimbabwe hasa kutokana na uzoefu wa Tanzania kupambana na mlipuko wa ugonjwa huo hasa katika Jiji la Dar-es-Salaam.

No comments:

Post a Comment