Wednesday, December 24, 2008

Ivo hayumo Chalenji

Kocha Mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars na timu ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Marcio Maximo, `amemtosa` aliyekuwa kipa wake namba moja kwenye kikosi cha timu hiyo, Ivo Mapunda, anayechezea St.George ya Ethiopia.

Maximo, toka achukue jukumu la kukinoa kikosi cha Stars miaka miwili iliyopita alikuwa akimuita Ivo mara kwa mara kwenye kikosi chake, ambapo hii ni mara yake ya kwanza kumuacha kipa huyo kwenye kikosi chake kinachotarajia kushiriki kwenye michuano ya kuwania Kombe la Chalenji, iliyopangwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu nchini Uganda.

Awali, Maximo alimuacha Ivo, baada ya kumjumuisha kwenye kikosi chake kilichokuwa kikijiandaa na mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya timu ya taifa ya Msumbiji,uliochezwa jijini Dar es Salaam, ambapo kipa huyo kwa mara ya kwanza alishindwa kuungana na wenzake kambini bila taarifa yeyote kitendo kilichomfanya Maximo kuchukua hatua ya kumpa nafasi Shaban Dihile kama kipa wa kwanza.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicolaus Musonye juzi lilitoa orodha ya wachezaji wa Kilimanjaro Stars na jina la Ivo lilikuwemo.

Akizungumza na Nipashe jana, Maximo alisema kuwa ameamua kumuacha Ivo kwenye kikosi chake hicho kutokana na kutojua mwenendo wa mchezaji huyo kwa sasa.

Aidha, Maximo amemuita kwenye kikosi chake mchezaji wa kimataifa anayecheza soka la kulipwa nchini Kuwait, Danny Mrwanda, ambapo alisema lengo la kumuita Mrwanda ni kutaka kukiongozea nguvu kikosi cha Kilimanjaro.

Alisema Mrwanda anayo haki ya kulitumikia taifa lake kwenye michuano hiyo kutokana na kutokuwepo kwa kipengele kinachomzuia mchezaji wa kimataifa kucheza, ambapo alisema kuwa wakati wowote kuanzia leo mchezaji huyo atatua nchini.

Maximo, anayeondoka nchini leo kwenda Ivory Coast, kushiriki katika zoezi la upangaji wa ratiba ya michuano ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani, ameteua jumla ya wachezaji 20, watakaoelekea Uganda, Jumanne ijayo kushiriki michuano hiyo.

Aliwataja wachezaji aliowachagua kuwa ni Shaban Dihile, Deo Mushi, Shadrack Nsajigwa, Kelvin Yondan, Salum Swed, Meshack Abel,Amir Maftah, Juma Jabu, Godfrey Bony, Shaban Nditi, Nurdin Bakar, Nizar Khalfan,Athuman Idd, Haruna Moshi, Kigi Makassy, Henry Joseph, Mrisho Ngasa, Musa Mgosi, Jerry Tegete na Danny Mrwanda.

Maximo, aliongeza kuwa pamoja na kukosa muda wa kutosha wa maandalizi ana uhakika wa kufanya vizuri, ambapo pia ataitumia michuano hiyo kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Ivory Coast, itakayofanyika mwishoni mwa mwezi Februari mwaka 2009.



Source: Nipashe

No comments:

Post a Comment