Wednesday, December 10, 2008

Raundi ya pili ya uchaguzi Ghana

Uchaguzi wa rais nchini Ghana sasa utaamuliwa kupitia raundi ya pili.

Habari hizo zimetangazwa na tume ya uchaguzi nchini Ghana.

Tume imeelezea kwamba mgombea wa chama kinachoiongoza serikali, Nana Akufo-Addo, amepata asilimia 49.13 ya kura, huku mpinzani wake John Atta Mills akipata asilimia 47.92 ya kura zote.

Hata hivyo hakuna aliyepata moja kwa moja asilimia 50 ya kura ili kutangazwa mshindi.

Kutokana na hali hiyo, raundi ya pili ya uchaguzi itafanyika tarehe 28 mwezi huu wa Desemba.

Maafisa nchini Ghana na vile vile wale wa kimataifa waliosimamia uchaguzi huo wameisifu nchi hiyo, kutokana na namna uchaguzi huo ulivyoendeshwa kwa hali nzuri kabisa.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, Kwadwo Afari Gyan aliuelezea mkutano na waandishi wa habari kwamba "kutakuwa na raundi ya pili ya uchaguzi, na itakuwa ni kati ya wagombea wawili wenye kura nyingi".

Zaidi ya asilimia 69.52 ya raia wa Ghana waliojiandikisha kupiga kura walishiriki katika uchaguzi huo wa tano wa Ghana, tangu ilipoanza kushiriki katika demokrasia ya mfumo wa vyama vingi vya kisiasa mwaka 1992.

No comments:

Post a Comment