Thursday, January 1, 2009

JK aelezea yaliyomuudhi na kumfurahisha 2008, atoa onyo 2009

Raisi Jakaya Kikwete ametoa onyo kali kwa wanasiasa wanaojihusisha na vitendo vya kuchochea ghasia nchini, akisema "tusije tukalaumiana".

Raisi alitoa onyo kali hilo katika hotuba yake ya salamu za mwaka mpya 2009 kwa wananchi, aliyoitoa jana kupitia vyombo vya habari, akizungumzia changamoto kadhaa za mwaka 2009 na mikakati ya serikali yake kukabiliana nazo baada ya mikakati ya mwaka 2008 kuathiriwa na kuporomoka kwa uchumi wa nchi tajiri kutokana na kuyumba kwa taasisi za kifedha.


"Tuache vitendo vya kuchochea ghasia kwa kisingizio chochote kile. Vitendo hivyo havitavumiliwa hata kidogo. Ni vizuri tukaambiana mapema tusije tukalaumiana," alisema Rais Kikwete ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2010.

"Tunaumaliza mwaka nchi ikiwa tulivu. Hii inathibitisha kuwa nchi inaweza kuwa tulivu isipokuwa pale ambapo baadhi yetu tutakapokuwa tumeamua kuwa isiwe hivyo. Naomba mwaka 2009 uwe tofauti.

"Naomba Watanzania wenzangu wote na hasa wanasiasa wenzangu tuyatambue hayo na tujiepushe nayo. Naomba makundi ya kijamii yatambue ukweli huo na waache kuwaendekeza wanasiasa hasidi."

Raisi Kikwete hakutoa ufafanuzi wa kauli hiyo nzito, lakini mwanzoni mwa hotuba yake alidokeza tu kwamba kulikuwa na vitendo vilivyoashiria "kuipeleka nchi kubaya".

"Ni ukweli ulio wazi kuwa katika mwaka huu tunaoumaliza sasa baadhi yetu tumekuwa tunafanya vitendo au kutoa kauli ambazo zilikuwa zinalielekeza taifa kubaya," alisema Kikwete. "Tena tulikuwa tunafanya hivyo kwa ajili ya kuendeleza manufaa binafsi ya kisiasa.

Ni matumaini yangu kuwa tutajiepusha na mambo hayo katika mwaka 2009. Nawasihi viongozi wenzangu wa kisiasa na wa kijamii tubadilike, tuweke mbele maslahi ya taifa ili tuiepushe nchi yetu na mabalaa ambayo baadhi ya wenzetu yaliwakuta."

Katika mwaka 2008 uliomalizika jana taifa lilishuhudia matukio mbalimbali- maandamano na migomo ya wafanyakazi, wanafunzi wa vyuo vikuu, wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, mapigano ya kikabilila mkoani na fujo katika kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Tarime mkoani Mara.

Baadhi ya vurugu hizo zilihusishwa na vyama vya kisiasa, ingawa havikuwekwa bayana kama ambavyo Raisi Kikwete hakuweka bayana vitendo hivyo vya uchochezi vilifanywa na watu gani.

Wakati fulani wanafunzi wa sekondari waliandamana hadi ofisi ya mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, wakirusha maneno makali dhidi ya serikali, wakidiriki kuiita kuwa ni ya kisanii.

Akizungumzia mauaji ya albino Raisi Kikwete alisema serikali inaendelea na mapambano kuhakikisha inatokomeza mauaji hayo na kwamba imeunda kikosi kazi kuendesha mapambano hayo.

Tayari watu 91 wamekamatwa na kufikishwa mahakamani. "Tumeunda kikosi-kazi kinachojumuisha Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa cha kuendesha mapambano haya," alisema Kikwete.

"Hivi sasa wanaendelea na uchunguzi wa kina nchi nzima kuwatambua wahalifu na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria."

Alisema mauaji hayo ni ya mateso na hayana sababu ya kwa kuwa chanzo chake ni cha kipuuzi na kwamba wanaoamini kuwa wakipata viungo vya albino watatajirika, waganga na wauaji serikali itawabana.

Akizungumzia hali ya uchumi alisema "kwa jumla hali ya uchumi wa nchi yetu kwa mwaka 2008 ilikuwa ya kiwango cha kuridhisha. Lakini, hali ingekuwa bora zaidi kama uchumi wa dunia usingepata misukosuko."

Alisema kutokana na hali hiyo baadhi ya malengo ya taifa kuhusu ukuaji na mwenendo wa uchumi wetu yameathiriwa na kusababisha matatizo mbalimbali ikiwemo mfumuko wa bei za mafuta na vyakula zilizopelekea kuongezeka kwa ukali wa maisha ya wananchi, idadi ya watalii kupungua nchini, bei za vyakula duniani kupanda hali itakayosababisha upungufu wa ajira katika mwaka 2009.

Alisema serikali itatumia nguvu nyingi katika kuhami na kukuza uchumi na kwamba serikali itaendelea kushirikiana na Benki Kuu kuzuia athari za soko la fedha duniani zisilifikie taifa na iwapo zitalifikia, makali yake yawe nafuu.

Akizungumzia matokeo ya darasa la saba Kikwete alisema matokeo hayo si ya kuridhisha katika miaka miwili iliyopita na kuwa ameiagiza wizara husika kufanya uchunguzi wa sababu za kushuka kwake, pamoja na kuzitafutia ufumbuzi, kazi ambayo itasimamiwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Akizungumzia suala la ATCL Raisi pia alisema serikali imekusudia kulifanyia marekebisho shirika hilo katika mwaka 2009, ili liweze kutoa huduma ipasavyo. "Yapo matatizo ya uendeshaji ambayo yamesababisha huduma zitolewazo ATCL kuwa za kiwango kisichoridhisha,” alisema Rais Kikwete.

"(2009) Tutafanya kila tuwezavyo kurekebisha mambo ili huduma hizo ziboreshwe na kuwafanya watumiaji kufurahi." Rais alitaja taasisi nyingine za umma ambazo utendaji wake ulikuwa mbaya ni Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).

"Katika mwaka 2009 tutaendelea kufuatilia na kusimamia kwa karibu hali katika mashirika ya reli, bandari na shirika la ndege," aliahidi Kikwete

No comments:

Post a Comment