Sunday, January 25, 2009

Timu za Zanzibar kuchezea mechi zake Dar

Wakati wawakilishi wa Tanzania Bara katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga wanatarajia kucheza na timu ya Comoro, Etoile D'or Mirontsy Januari 31 kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, nalo shirikisho la soka Afrika (CAF) limeziruhusu timu za Miembeni na Mundu za visiwani Zanzibar kutumia kiwanja hicho kwenye michuano hiyo.

Michuano hiyo ya Afrika ngazi ya vilabu inayoandaliwa na (CAF) inatarajia kuanza kutimua vumbi mwishoni mwa juma lijalo huku Tanzania ikiwa na wakilirishi wanne timu mbili kutoka Bara na mbili kutoka Visiwani.

Akizungumza na waandishi wa habari Afisa habari wa shirikisho la soka nchini (TFF) Florian Kaijage alisema tayari shirikisho hilo limewasilisha taarifa kuwa mchezo wa marudiano utafanyika Comoro kama ratiba ilivyopangwa.

Alisema kwa sasa kuna uwanja ambao ulikwishakaguliwa na kuthibitishwa na shirikisho la soka duniani FIFA kwa ajili ya michuano hiyo.

Kaijage alisema timu ya Prison ambao wanawakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho wao watacheza mchezo wao dhidi ya Khalij Sert ya Libya, Februari mosi.

Alisema waamuzi wa mchezo huo wanatoka nchini Kenya ambao ni Alfred Ndinya, Wamalwa Elias pamoja na Sagero David na mwamuzi wa akiba akitokea Tanzania, Ali Kombo.

Aidha wapinzani hao wa Tanzania Prisons wanatarajia kuwasili nchini Alhamisi kwa ndege maalamu, na TFF wakiahidi kufuatilia kwa karibu maendeleo ya wawakilishi hao wa nchi ili waweze kupata matokeo mazuri.

"Tutahakikisha timu zetu zinashiriki vizuri katika michezo hii ya ngazi za klabu na tutakuwa nao bega kwa bega kuhakikisha wanafanya vizuri kwa maendeleo ya mpira hapa nchini,"Alisema Kaijage.

Wakati huo huo imeripotiwa kuwa CAF imezikubalia timu za Miembeni na Mundu kutumia Uwanja wa Taifa wa jijini Dar es salaam kwenye mechi zao za michuano ya Afrika.

Hatua hiyo imekuja baada ya uwanja Amani kuwa na ukarabati na ule wa Gombani unawekwa nyasi za bandia.

Akizungumza jana msemaji wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) Hafidh Ally alisema kuwa baada ya kukubaliwa na CAF na taratibu zingine za kuhakikisha timu hizo zinafanya vizuri katika michuano hiyo.

"Tunaendelea na mikakati ya kuhakikisha timu zetu ambazo zinaipeperusha bendera ya Zanzibar katika michuano ya kimataifa ziweze kufanya vizuri.

"Pia tunajipanga kuhakikisha taratibu zote ambazo zinahusiana na mashindano hayo zinakwenda sawa bila ya matatizo."

Alisema ZFA ndiyo itakayokuwa ikihusika na Taratibu zote katika mechi zote zinazo husisha timu hizo kama taratibu za CAF zinavyosema.

"ZFA ndiyo hasa itakuwa inahusika katika mechi hizo ikiwa ni pamoja na kupanga viingilio vya mechi.

"Kama kutakuwa na taratibu nyingine zinazohitaja ufafanuzi basi moja kwa moja tutawasiliana na CAF," alisema.

Timu ya Miembeni inashiriki michuano ya Klabu bingwa Afrika wakati timu ya Mundu yenyewe inashiriki michuano ya Shirikisho.


No comments:

Post a Comment