Tuesday, January 27, 2009

CUF wagomea matokeo ya ubunge Mbeya Vijijini

WAKATI Tume ya Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbeya Vijijini ikimtangaza mgombea ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mchungaji Luckson Mwanjali kuwa mshindi, Chama cha Wananchi (CUF), kimeyakataa matokeo hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya matokeo ya awali kutangazwa, Mwenyekiti wa CUF, Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba alisema chama chake hakiyatambui matokeo hayo kutokana na kuwepo kwa kasoro nyingi kuanzia wakati wa kampeni na siku ya upigaji kura.

Alisema matatizo ya awali ni pamoja na kampeni za CUF kuingiliwa na viongozi wa kampeni na kutoa mfano kuwa, katika kata ya Ikukwa baada ya chama hicho kufanya mkutano wao, CCM walitumia watu hao hao waliokuwa katika mkutano huo, jambo ambalo ni kinyume na utaratibu wa kampeni za uchaguzi.

"Kwa mfano katika kijiji cha Ikukwa ilikuwa ni siku ya chama chetu kufanya mkutano hapo na CCM ikawa na ratiba katika eneo hilo. Lakini cha kushangaza tulipomaliza mkutano wetu na wao wakaingia na kufanya mkutano katika eneo hilo hilo ambalo sisi tulikuwa tumewakusanya watu," alilalamika Lipumba.

Alisema kuwa matatizo mengine ni pamoja na kupigwa kwa mwanachama wao na wafuasi wa CCM, kushushiwa bendera pamoja na kuchana picha ya mgombea wao.

Hata hivyo, alisema CCM waliomba msamaha baada ya suala hilo kufikishwa Tume ya Uchaguzi na kuzikutanisha pande zote mbili.

Profesa Ibrahim alisema kuwa, tatizo kubwa ambalo ndilo lililochangia watu wachache kutojitokeza kupiga kura ni watendaji wa vijiji na kata kuzuia shahada za wapigakura kwa kisingizio cha kuwapa vocha za mbolea ya ruzuku.

"Tatizo kubwa ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa wananchi kutopata haki ya kupiga kura, ni watendaji wa baadhi ya vijiji waliohodhi shahada za kupigia kura za wananchi kwa madai kuwa watapata vocha ya mbolea ya ruzuku," alisema na kuongeza:

"Mwananchi wa Kijiji cha Msituni, Kata ya Iwindi, Ezekieli John alituambia kwamba hawezi kupiga kura kwa sababu shahada yake ilichukuliwa na balozi wa nyumba kumi na taarifa hiyo tumeipeleka polisi," alilalamika Profesa Lipumba.

Mwenyekiti huyo alibainisha matatizo yaliyojitokeza siku ya kupiga kura kuwa ni pamoja na vituo vingi kutokuwa na majina ya wapigakura na kwamba, hata sehemu ambayo yalibandikwa hayakuwa sahihi.

Aliongeza kuwa, katika baadhi ya vijijini vya kata za Ilembo na Santilya vituo vilikuwa na umbali wa kilomita saba hadi kumi kutoka maeneo wanayoishi wananchi, hivyo kusababisha baadhi yao kushindwa kupiga kura.

"Siku ya kupiga kura tulifanikiwa kuwakamata vijana wakiwa na masanduku ya kupigia kura, hivyo hayo yote ni mlolongo wa kasoro ambazo zimejitokeza na kutufanya sisi tusiyakubali matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi," alisema.

Alisema kuwa kwa sasa wanaandaa utaratibu wa kuwasiliana na wanasheria wa chama chao ili kupata ushauri wa hatua za kuchukuliwa.

Alilalamika kuwa, kuna tatizo kubwa la kiutendaji ndani ya tume, kwani watendaji wake waandamizi wako Dar es Salaam badala ya kuwepo maeneo yote ya wapigakura ili kubaini matatizo hayo mapema.

"Unajua, tume haiwezi kumwadhibu mkurugenzi wa wilaya ambaye ndiye msimamizi wa uchaguzi kwa kuwa yeye si mwajiriwa wa tume, bali ni mkubwa wake wa kisiasa ambaye ni mkuu wa Wilaya ambaye ana uwezo kumshawishi atakavyo, ikiwamo kuhakikisha CCM inapata ushindi," alisema.

Profesa Lipumba alisema kuwa, kuna umuhimu mkubwa wa kuwepo kwa tume huru ambayo itaweza kufanya kazi kwa kuhakikisha inafika maeneo ya vijijini ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya uraia ili wananchi wote wapate haki ya kupiga kura.



No comments:

Post a Comment