Sunday, January 4, 2009

Atta Mills ashinda uchaguzi Ghana


Wafuasi wa rais Mteule John Atta Mills

Mgombea wa upinzani John Atta Mills ameshinda uchaguzi wa urais nchini Ghana , kwenye mchuano mkali wa marudio ya kura .

Tume ya uchaguzi ya Ghana imemtangaza Bwana Atta Mills kuwa mshindi baada ya matokeo ya jimbo la mwisho kuonyesha anamzidi mpinzani wake wa chama tawala Nana Akufo- Addo kwa wingi wa kura.

Chama tawala kilisusia upigaji kura katika jimbo hilo la Tain siku ya Ijumaa.

Pande zote mbili zimetoa madai ya wizi wa kura. Jamii ya kimataifa ilikuwa inafuata kwa karibu sana marudio ya uchaguzi huo, kwa kuwa Ghana ni mfano bora wa demokrasia katika Afrika ya magharibi.

Tume ya uchaguzi imesema matokeo ya marudio hayo yameonyesha Bwana Atta Millls alipata ushindi mwembamba wa asilimia 50.23% ya kura zote , huku mpinzani wake Akufo -nAddo akipata asilimia 49.77% .

Bwana Akufo-Addo alishinda duru ya kwanza, lakini ushindi huo haukutosha kuepuka marudio.

Mkuu wa tume ya uchaguzi amesema tume hiyo imeyazingatia madai ya wizi wa kura yaliyotolewa na pande zote , lakini haikupata ushahidi wa kutosha kubatilisha matokeo.

Rais anayeondoka John Kufuor awali alitoa wito kwa wagombea wote wawili kuheshimu matokeo.

Alitoa wito wa kuwepo kwa utulivu, na akasema malalamiko yoyote ya wizi wa kura yanatakiwa kushughulikiwa na mahakama baada ya rais mpya kuapishwa siku ya jumaatano.

Kumekuwa na shangwe na nderemo katika makao makuu ya chama cha Bwana Atta Mills cha National Democratic Congress .

Mwandishi wa BBC anasema ingawa kunakuwa na mgawanyiko mkubwa sana nchini Ghana wakati wa kuchagua rais, nchi hiyo imedhibitisha kwamba Demokrasia inawezekana.

Bwana Atta Mills ana umri wa miaka 64 , na alikuwa makamu wa rais wa Ghana zamani. Ameshindwa mara mbili kwenye uchaguzi wa urais na rais John Kufuor.

Wachambuzi wanasema uchaguzi wa Ghana huenda ukarejesha heshima ya demokrasia ya kikatiba barani Afrika, kufuatia uchaguzi uliozua utata nchini Kenya na Zimbabwe mwaka uliopita, na mapinduzi ya kijeshi nchini Guenea na Mauritania.

Matumaini zaidi yameongezeka kwenye uchaguzi huu kwa kuwa Ghana imegundua kwamba inayo mafuta ambayo yataanza kuiletea nchi pato kuanzia mwaka ujao wa 2010.


Source: BBC

No comments:

Post a Comment