Thursday, January 22, 2009

Yanga na Simba zafanya kweli ligi kuu

Timu za soka za Yanga na Simba jana ziliibuka na ushindi katika mechi za Ligi Kuu walizocheza kwenye viwanja tofauti. Simba iliyokuwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam iliichapa Villa Squad kwa mabao 2-0 wakati Yanga ambayo ilisafiri hadi Uwanja wa Sokoine Mbeya iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Prisons.

Baada ya kosakosa za hapa na pale, vijana hao wa mtaa wa Msimbazi wanaonolewa na Mzambia Patrick Phiri, walipata bao katika dakika ya 22, bao lililofungwa na Mussa Hassan ‘Mgosi’aliyeunganisha krosi ya Ulimboka Mwakingwe ambaye naye alipokea pande la Juma Nyosso aliyepanda mbele kusaidia mashambulizi.

Kwa matokeo hayo yameiwezesha Simba kuchupa kutoka nafasi ya sita katika msimamo wa ligi hadi nafasi ya nne, ikiwa na pointi 20 nyuma ya Mtibwa Sugar kwa pointi moja iliyofikisha pointi 21, Kagera Sugar yenye pointi 23 iko nafasi ya pili nyuma ya Yanga inayoongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 36.

Katika mchezo huo wa jana, Simba na Villa walianza mchezo huo kwa kasi na endapo washambuliaji wake wangekuwa makini pengine hadithi ingekuwa tofauti kwani pamoja na kufungwa vijana wa Villa walionekana kucheza vyema lakini umaliziaji ulikuwa mbovu.

Dakika moja baadaye shuti la Nassoro Said ‘Cholo’ lilitoka nje kidogo ya lango, baada ya Ulimboka Mwakingwe, Jabir Azizi na Nico Nyagawa kugongeana vizuri. Villa walijaribu kujitutumua na kujibu shambulizi hilo katika dakika ya 25 na kupata kona ambayo ilichongwa na Yusuph Gogo na kuokolewa na walinzi wa Simba ambao walikuwa wakiongozwa vyema na Juma Saidi ‘Nyosso’ kulilinda lango lao.

Katika dakika ya 31 ya mchezo Simba walifanya mabadiliko kwa kumwingiza Henry Joseph badala ya Mohamed Banka ili kuimarisha safu yake ya kiungo ambayo ilionekana kulegalega kidogo wakati Villa walimwingiza Iddi moshi badala ya Mussa Nampaka.

Baada ya bao hilo Simba waliongeza kasi na kuwafanya walinzi wa Villa kuwa na kazi ya ziada kuwakabili lakini washambuliaji wa Simba bado hawakuwa makini zaidi kupachika mabao zaidi.

Pande zote mbili zilifanya mabadiliko kwa Simba kuwaingiza Orji Obina, Adam King’wande badala ya Ramadhan Chombo na Jabir Aziz ambaye kabla ya kutoka alikuwa ameumizwa, Villa wao waliwaingiza Lameck Daiton, Jackson Chikwela badala ya Athumani Kibarati na Ally Kulwa, mabadiliko yaliyoonekana kuinufaisha zaidi Simba .

Matokeo hayo si mazuri kwa Villa, kwani imebaki nafasi ya 11 kati ya timu 12 zinazoshiriki ligi hiyo, ikiwa na pointi zake 11 na ina michezo tisa mkononi imalize ligi hiyo ambayo itashuhudia timu tatu za mwisho zikishuka daraja.

Hata hivyo, Kocha wa Villa Kennedy Mwaisabula alijinasibu kuwa timu hiyo ipo imara na itafanya vyema katika michezo yake iliyosalia, na haitoshuka daraja kama watu wengi wanavyodhania kwani ina mechi nyingi za nyumbani ambazo ana hakika vijana wake watafanya maajabu. Kutoka Mbeya inaripotiwa, bao la Yanga lilifungwa katika dakika ya 76, bao hilo lilifungwa na Athumani Idd aliyeunganisha krosi ya Mrisho Ngassa liliipa Yanga ushindi wa 1-0 dhidi ya Prisons.



No comments:

Post a Comment