Timu ya soka ya Taifa ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars', jana ilijiweka katika mazingira mazuri zaidi ya kufuzu nusu fainali ya michuano ya Kombe la Chalenji inayoendelea nchini Uganda, baada ya kuinyuka Rwanda 'Amavubi' kwa mabao 2-0.
Mechi hiyo ya Kundi A, ilifanyika Uwanja wa Nakivubo. Wakati Stars ikiiangamiza Rwanda, timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’ iliifunga Somalia kwa mabao 4-0, hivyo kufikisha pointi saba na kuendelea kuongoza kundi hilo, ikiwa imejiweka katika asilimia kubwa ya kufuzu hatua ya nusu fainali.
Uganda itamaliza mechi za makundi kesho kwa kucheza na Stars yenye pointi sita kutokana na michezo mitatu iliyocheza. Stars inayonolewa na Mbrazili Marcio Maximo ilipachika bao la kwanza dakika ya nane, mfungaji akiwa Mrisho Ngassa, aliyeunganisha pasi ya Haruna Moshi 'Boban’ na mpira kumkuta mfungaji aliyeutumbukiza wavuni.
Kabla ya bao hilo lango la Rwanda ambayo mchezo wa kwanza ilinyukwa kwa mabao 4-0 na Uganda, kabla ya kuifunga Somalia mabao 3-0, lilikuwa katika hekaheka, lakini Danny Mrwanda na Athumani Idd 'Chuji' kwa nyakati tofauti walishindwa kulenga lango.
Rwanda nayo ilipata nafasi kadhaa za kufunga, lakini Tuyisenge Pekeyake, Kamana Bakota, Ntaganda Elias kwa nyakati tofauti, mikwaju yao ilitoka nje ya lango, au iliokolewa na kipa Deogratius Munishi wa Stars.
Dakika ya 37 Idd alipachika bao la pili kwa shuti, likiwa pia ni bao lake la pili katika michuano hiyo, baada ya Jumatatu kufunga bao moja katika ushindi wa mabao 2-0 uliopatikana kwenye mechi dhidi ya timu ya Taifa ya Zanzibar 'Karume Boys’.
Mabadiliko yaliyofanywa na Maximo kipindi cha pili kuwatoa kwa nyakati tofauti Idd, Ngassa na Moshi na kuwaingiza Mussa Hassan 'Mgosi', Nurdin Bakari na Nizar Khalfan, yaliisaidia kwa kiasi kikubwa Stars kuendelea kumiliki mpira, ingawa umaliziaji bado ulikuwa tatizo.
Katika kipindi hicho, Mgosi, Mrwanda na Nizar waliingia mara kadhaa katika eneo la hatari la Rwanda, lakini walishikwa na vigugumizi vya miguu na kushindwa kuliona lango. Kwa matokeo hayo, Stars imefikisha pointi sita, ikiwa na mchezo mmoja mkononi dhidi ya Uganda 'The Cranes' kesho.
Lakini kwa kipigo cha jana, Rwanda sasa ili isonge mbele, itabidi iifunge Zanzibar kesho, huku ikiomba Stars ifungwe na kusubiri uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa. Katika mchezo mwingine jana alasiri, Uganda na Somalia, mabao ya washindi yalifungwa na Tonny Maweje (dakika ya 31 na 65), Owen Kasule (dakika ya 39) na Maasa Godfrey (dakika 74).
Uganda sasa ina pointi saba na mabao manane, hivyo kama Stars itaifunga Uganda kesho itafikisha pointi tisa na kushika nafasi ya kwanza, lakini bado Uganda itasonga mbele kutokana na wingi wa mabao ya kufunga, labda Zanzibar yenye pointi nne na mabao matatu kushinda mechi yake ya mwisho kwa mabao zaidi ya saba.
Zanzibar imefungwa mabao mawili na Uganda haijafungwa bao lolote mpaka sasa. Lakini Zanzibar pia inaweza kufuzu kama Stars itafungwa, halafu yenyewe ikaifunga Rwanda. Wakati huohuo, michuano hiyo inaendelea leo kwa Kundi B, ambapo Zambia itaumana na mabingwa watetezi Sudan mchana, kisha alasiri Kenya na Burundi kwenye uwanja huo huo.
No comments:
Post a Comment