Friday, January 2, 2009

Raisi Karume atangaza vita ya ufisadi Zanzibar

Raisi wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, amesema miongoni mwa malengo makuu ya serikali yake katika mwaka huu wa 2009 ni kupambana na ubadhirifu na matumizi mabaya ya rasilimali za umma.

Akitoa salamu za mwaka mpya na kuuaga mwaka 2008 katika Ikulu ya Zanzibar, Raisi Karume alisema hatua hizo lazima zichukuliwe ili kulinda mali za wananchi, na serikali itahakikisha wote wanaopaswa kulipa kodi wanalipa ipasavyo.

Alisema kwamba hatua hizo ni muhimu kuchukuliwa kwa vile pia zitasaidia kukabiliana na mgogoro wa kifedha unaozikumba nchi za Ulaya na Marekani, ambazo athari zake zinaweza pia kuyumbisha mataifa yanayoendelea.

“Sisi sote tunawajibu wa kujiweka vyema tusikumbwe na dhoruba hizo, miongoni mwa mambo ya kuazimia kuyafanya mwaka ujao ni kutunza matumizi yetu na kuepukana na ubadhirifu na kulinda mali za umma,” alisema Raisi Karume.

Hata hivyo alisema watendaji waliopewa jukumu la kukusanya kodi wanawajibika ipasavyo ili kuhakikisha mapato hayapotei.

Kauli hiyo ya Raisi Karume imekuja huku kukiwa na malalamiko kwamba serikali imekuwa haionyeshi makucha katika kupambana na vitendo vya ufisadi na rushwa, kama ilivyojitokeza katika Serikali ya Muungano.

Aidha, Raisi Karume alisema serikali imejipanga kuhakikisha sekta ya kilimo inapata mafanikio makubwa, kama utekelezaji wa maazimio ya Shirika la Chakula Duniani (WFP) na Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Zanzibar (MKUZA).

Alisema serikali itahakikisha inawapatia wakulima mbegu bora zilizofanyiwa utafiti ili kuongeza uzalishaji na kuwapatia mbolea wakulima kwa gharama nafuu.

Haya ni katika maazimio yetu ya mwaka mpya ambayo ni miongoni mwa malengo ya maendeleo ya milenia ya kuwapatia mafunzo ya ukulima bora wananchi ili waweze kuendeleza sekta hiyo.

Wakati huo huo, Raisi Karume amewataka wananchi kutoa ushirikiano ili kuhakikisha kazi ya uandikishaji wapiga kura katika daftari la kudumu inafanikiwa, kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao visiwani humu.

Zoezi la uandikishaji wapiga kura katika daftari la kudumu Zanzibar linatarajiwa kuanza mwezi huu, baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kudai shahada zilizotumika katika uchaguzi mkuu uliopita hazifai, kwa kuwa zilitengenezwa chini ya kiwango cha ubora.

“Wakati zoezi la utayarishaji daftari la kudumu la wapiga kura likiendelea, tushirikiane sote kuimarisha kazi hiyo ili tufanikiwe kustawisha demokrasia na haki za watu wote kwa salama na amani,” alisema Raisi Karume.

No comments:

Post a Comment