Saturday, January 10, 2009

Sheikh Yahya si Mungu - CCM

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeuponda utabiri uliotolewa juzi na Mnajimu Sheikh Yahya Hussein na kusema, sheikh huyo sio Mungu kutabiri mpasuko ndani ya chama hicho.

Katibu Mkuu Yusuf Makamba alisema jana kuwa, CCM haiwezi kuvunjwa moyo na utabiri huo kwa kuwa Sheikh Yahya ni binadamu anayeweza kutumia busara zake kusema anachoamini kuwa kweli.

Kauli ya Makamba imekuja siku moja baada ya Sheikh Yahya Hussein kuitabiria CCM mpasuko na kueleza kuwa Serikali itakayoundwa mwakani, itakuwa ya umoja wa vyama vya siasa.
Sheikh Yahya alisema CCM mwakani haitakuwa na nafasi kutawala peke yake ingawa Rais Jakaya Kikwete bado ataendelea na wadhifa wake wa urais.


"Siwezi kukubaliana na utabiri wa Sheikh Yahya kwa sababu yeye sio Mungu na kama watu wanaweza kuamini utabiri wake na kukubaliana nao basi. Mimi pia ninatabiri kwamba CCM haitapasuka bali itaendelea kutawala nchi hii milele," alisema Makamba kwa kejeli.

Kwa mujibu wa Makamba, CCM bado ni chama imara na kamwe hakiwezi kupasuka kama Sheikh Yahya anavyosema katika utabiri wake na pia serikali yake itakayoiunda mwakani itaendelea kuwa ya chama kimoja.

"Kama Sheikh Yahya ametoa utabiri huo na mimi ninatabiri hivyo sasa tuone nani mkweli katika utabiri wake," alisema Makamba na kuongeza: "Huu sio wakati wa kutabiri ni wakati wa kuzungumzia maendeleo ya chama lakini kama unaona suala la utabiri wa Sheikh Yahya ndiyo la muhimu, ukaandike kwamba Makamba kasema Sheikh Yahya sio Mungu na siwezi kukubaliana na utabiri wake."

Alifafanua kwamba CCM haiwezi kuyumba kwa sababu yoyote na itaendelea kutawala bila kushirikiana na vyama vingine. Sheikh Yahya pia katika utabiri wake alisema uchaguzi wa mwaka 2010 hautakuwa na wizi wa kura kwa kuwa watu wamekuwa wajanja na vyama vya siasa nchini vina nguvu sana.

Alifafanua kuwa, Serikali ya mwaka 2010 ni ya muungano wa vyama, uchaguzi ujao hautakuwa na wizi wa kura kama vile ilivyokuwa awali, vyama vya Upinzani kulaumiana na chama tawala. Kwani utajiri na mali ni kigezo cha kupatikana Serikali ya vyama vyote.

Sheikh Yahya alisema kila kitu kina dalili zake na kwamba dalili ya CCM kukwama katika uchaguzi wa 2010 zimekwishaonekana. Suala la CCM kushirikiana na Chama cha Demokrasia (DP), katika uchaguzi mdogo wa Tarime ni udhaifu na dalili tosha juu ya kushindwa kwake," alisema Sheikh Yahya.

Alisema mpasuko ndani ya CCM umetokana na Rais Kikwete kuwa mpinzani mkubwa kwa watu, marafiki, viongozi na hata wanachama wenzake kutokana na kazi na ujasiri wake wa kushughulikia mafisadi ili kulinda mali za umma na kwamba hiyo ndiyo sababu ya kumrudisha madarakani 2010.

Source: dullonet

No comments:

Post a Comment