Sunday, January 4, 2009

Kilimanjaro Stars yaanza vibaya kombe la Challenge

Mchezaji wa zamani wa klabu ya Simba ya Dar es Salaam, Issa Abushir jana alikuwa mwiba kwa Kilimanjaro Stars na kusababisha kulala kwa bao 1-0 dhidi ya Somalia katika mchezo wa michuano ya Kombe la Cecafa inayoendelea Kampala, Uganda.

Bao la dakika ya 13 la Abushir liliiwezesha Somalia kuibuka na ushindi huo wa kushangaza dhidi ya Stars katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Nakivubo, Kampala, jana katika michuano hiyo ya nchi 10 inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka kwa Nchi za Afrika Mshariki na Kati (Cecafa).

Abushir aliandika bao hilo pekee kutokana na mpira wa faulo ambao mabeki wa Kilimanjaro Stars walizembea wakidhani ameotea, lakini mwamuzi Ali Farah wa Djibouti hakupiga filimbi hivyo mfungaji kuachia shuti lililomshinda kipa namba moja wa Stars, Juma Dihile.

Kipigo hicho ni cha aibu kwa Kilimanjaro Stars, timu inayoundwa na wachezaji wa Taifa Stars ambao wanapewa nafasi kubwa ya kunyakua taji hilo kutokana na kuwa miamba katika ukanda wa Afrika Mashariki. Kipa wa Somalia, Khalid Ali alikuwa kikwazo kwa Stars baada ya kuokoa hatari kadhaa langoni mwake kipindi cha pili.

Matokeo hayo pia yanatia shaka kwa Kilimanjaro Stars kuendeleza mwenendo mbaya katika michuano hiyo ambayo mara ya mwisho walitwaa taji mwaka 1994. Jinamizi la Kilimanjaro Stars kwenye michuano ya Cecafa linaonekana kuendelea kuitesa na historia inaonyesha wanazinduka kila baada ya miaka 20 kutokana na pia kutwaa taji mwaka 1974.

Kocha wa Kilimanjaro Stars, Mbrazil Marcio Maximo akihojiwa na kituo cha redio cha TBC Taifa baada ya mechi hiyo alisema wamepata somo kutokana na makosa ya mechi hiyo. “Ni funzo kwa wachezaji kwa sababu walizembea kukaba wakidhani mfungaji ameotea, katika mchezo hutakiwi kuweka mawazo kama hayo.”

Lakini Maximo alisema kipindi cha pili vijana wake walicheza vizuri na kupeleka mashambulizi mengi langoni mwa wapinzani wao, hata hivyo, bahati ilikuwa upande wa Somalia. Kipigo hicho kinawaweka Stars njia panda wakati kesho wana mtihani mgumu dhidi ya Zanzibar ‘Karume Boys’ ambao mechi ya kwanza waliilaza Somalia kwa mabao 2-0 na jana walikuwa wakionyeshana kazi na wenyeji Uganda.

Kilimanjaro Stars pia wana kibarua dhidi ya Uganda na Rwanda katika mechi tatu zilizosalia za Kundi A na ushindi katika mechi hizo ndio utaiokoa na aibu ya kurudi nyumbani mapema. Uganda katika mechi ya kwanza waliilaza Rwanda kwa mabao 4-0 hivyo kutoa onyo kwa timu nyingine. Kilimanjaro Stars: Dihile, Shedrack Nsajigwa, Juma Jabu, Meshack Abel, Salum Sued, Godfrey Bonny, Mrisho Ngassa, Henry Joseph, Jerson Tegete/Danny Mrwanda, Nizar Khalfan/Musa Hassan ‘Mgosi’ na Nurdin Bakari/Athumani Idd.


No comments:

Post a Comment