Monday, January 12, 2009

Kilimanjaro Stars yafungwa 2-1 na Harambee Stars

Kilimanjaro Stars imeshindwa kung’ara, baada ya kuchapwa kwa mabao 2-1 na Kenya katika mechi ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Chalenji iliyofanyika jana.

Mechi hiyo ilifanyika saa 6:30 mchana kwenye Uwanja wa Nambole, Kampala, Kenya iliweza kusonga mbele baada ya kupata mabao ya harakaharaka yaliyofungwa ndani ya dakika tatu kwenye kipindi cha kwanza.

Stars ilipata bao katika dakika ya 77 lililofungwa na Danny Mrwanda baada ya kupokea krosi safi ya Mrisho Ngassa ambaye aliwapiga chenga mabeki watatu kutoka winga ya kulia na kumpatia mfungaji aliyeachia shuti lililokwenda kirahisi wavuni baada ya kumpita kipa Duncan Ochieng.

Baada ya bao hilo, mwamuzi kutoka Somalia Hassan Haile alimzawadia kadi nyekundu Salum Swedi ambaye aliangushwa na mchezaji wa Kenya, kadi iliyofanya Kilimanjaro Stars kumalizia dakika 13 za mwisho wakiwa pungufu.

Bao hilo pekee la Kilimanjaro Stars halikuweza kuisaidia kutinga fainali kufuatia mshambuliaji wa Azam FC, Francis Ouma kuipatia Kenya bao la kwanza dakika ya 19, baada ya kipa Shaban Dihile aliyekuwa mgonjwa kupishana na mpira.

Dakika tatu baadaye mshambuliaji wa Yanga Mike Barasa aliifungia timu yake bao la pili, akitumia makosa ya mabeki wa Kilimanjaro Stars. Sasa Kilimanjaro Stars itashuka dimbani kuwania nafasi ya tatu na kitita cha dola za Marekani 10,000 itakapoumana na Burundi iliyochapwa kwa mabao 5-0 na Uganda katika mechi ya pili ya nusu fainali.

Mechi ya jana iliyochezwa wakati kukiwa na jua kali iliwalazimu wachezaji wa timu zote mbili kufanya kazi ya ziada ya kujimwagia maji ili kupooza miili yao. Kilimanjaro Stars ilishuka dimbani ikiwakosa wachezaji wake nyota nahodha Shadrack Nsajigwa ambaye amekuwa akionyesha umahiri mkubwa katika safu ya ulinzi baada ya kupewa kadi mbili za njano, beki Kelvin Yondan aliyeonyeshwa kadi nyekundu kwenye mechi dhidi ya Uganda na Meshack Abel, ambaye ni majeruhi wa enka.

Kocha Mbrazil Marcio Maximo hakuwa na njia bali ni kubadilisha mfumo kwa kulazimisha kuwachezesha Nurdin Bakari upande wa kulia na kiungo Henry Joseph kucheza kama kiungo mkabaji, jambo ambalo lilifanya Stars kufungwa mabao mawili ya harakaharaka kipindi cha kwanza.

Kilimanjaro Stars ilionekana kubadilika pale Maximo alipoamua kuwaingiza Musa Hassan ‘Mgosi’ na Amir Maftaha akiwatoa Haruna Moshi na Athumani Iddi. Hata hivyo, kama mwamuzi Haile angechezesha kwa kufuata sheria 17 za soka, basi mambo yangeweza kuwa tofauti kwa Kilimanjaro Stars.

Mwamuzi huyo alishindwa kuamuru ipigwe penalti baada ya Mgosi kuangushwa eneo la hatari na nahodha Henry Ochieng na pale beki wa Kenya aliposhika mpira kwa makusudi. Kocha Maximo alisema, “Tulicheza vibaya katika kipindi cha kwanza lakini tulikuwa imara kipindi cha pili.

Ninawapongeza wachezaji wangu waliopigana kufa na kupona katika dakika za mwisho na sasa tunaelekeza nguvu kwenye mechi ijayo.” Maximo na Meneja wa timu Leopold Tasso Mukebezi walikataa kutoa shutuma kwa mwamuzi kama kisingizio cha kufungwa wakati wakihojiwa na TBC Taifa. “Siwezi kutoa maoni kuhusu mwamuzi. Kufungwa ni moja ya mchezo,” aliiambia TBC Taifa mara baada ya mechi.

No comments:

Post a Comment