Monday, January 5, 2009

Phiri arudi Simba

Kocha wa zamani wa Simba Partick Phiri aliwasili upya nchini jana Jumamosi lakini akasema hajafikia makubaliano yoyote ya kuifundisha timu hiyo.

Alisema amekuja kwa ajili ya mazungumzo na uongozi wa klabu yake hiyo ya zamani na leo Jumatatu ndiyo atakuwa katika nafasi ya kuzungumzia kama atakuwa mwalimu kwa kipindi cha tatu katika miaka minne.

Simba inayoshiriki Kombe la Mapinduzi la Zanzibar ipo chini ya beki wa zamani wa timu hiyo na Majimaji ya Songea Amri Said baada ya kumtimua Mbulgaria Krasimir Bezinski.

Phiri ambaye aliiongoza timu ya taifa ya Zambia kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kutoka Simba kwa mara ya pili 2006, na ambaye alitimuliwa baada ya Chipolopolo kutolewa katika hatua ya makundi ya fainali za Ghana mwaka jana:

Alisema amefurahia kurudi nchini kutokana na kupata marafiki wengi, na kwamba anategemea mazungumzo na Simba yatakwenda vizuri baada ya mawasiliano ya awali na uongozi wa klabu kwa njia ya simu.

Alisema anawakumbuka wachezaji Mussa Hassan `Mgosi` na Haruna Moshi ambao alikuwa nao wakati huo.

``Siwezi kuongea chochote kwa sasa, ndio nimefika na baada ya mazungumzo na kuiona timu nitaweza kuongea na waandishi labda Jumatatu,`` alisema Phiri ambaye ataondoka baadaye leo kwenda Zanzibar.

Naye mwenyekiti wa klabu hiyo Hassan Dalali ambaye aliyefika kumpokea kocha huyo alisema wamefurahia kuwasili kwa kocha huyo, na wana imani atadumu muda mrefu tofauti na walimu wa awali kutokana na kuyajua mazingira ya klabu yake.

Dalali ambaye timu yake imefundishwa na makocha wanne weupe na Twalib Hilal katika miaka miwili iliyopita aliwataka wapenzi na wanachama wa Simba kumpa ushirikiano kocha huyo.

Alisema atalipwa mshahara kutoka katika mgao wa fedha za udhamini wa Kampuni ya Bia.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati ya mashindano ya Simba, Othman Hassan `Hassanoo`alisema jana kwa njia ya simu kocha huyo atapimwa kutokana na timu kufanya vizuri kwenye ligi.

Endapo itaboronga hawatasita kumuondoa kama walivyoondolewa wengine.

Naider Dos Santos, Nilsen Elias, Milovan Cirkovic na Bezinski ndiyo wengine aliokuwa akizungumzia Hassanoo.


Source: Lete Raha

No comments:

Post a Comment