Monday, January 26, 2009

Lubanga akanusha mashtaka

Thomas Lubanga- amekanusha mashtaka ya kuandikisha watoto jeshini

Kiongozi wa zamani wa kundi la wapiganaji katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Thomas Lubanga amekanusha mashtaka ya kuwatumikisha watoto jeshini, mbele ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita (ICC).

Anakabiliwa na mashtaka sita ya kuwaandikisha na kuwatumia mamia ya watoto wa umri wa chini ya miaka 15 kupigana kwenye vita vya Congo vya miaka mitano , vilivyomalizika mwaka 2003.

Akifungua utaratibu wa kusoma mashtaka, kiongozi wa mashtaka wa mahakama hiyo Luis Moreno-Ocampo alisema Bwana Lubanga aliwatumia watoto ''kuuwa, kulemaza na kubaka.''

Hii ni kesi ya kwanza kusikilizwa mbele ya mahakama hiyo iliyoko The Hague.

Kesi hiyo imerejeshwa baada ya kucheleweshwa kwa muda wa miezi saba, huku majaji na viongozi wa mashtaka wakipinga ushahidi uliotolewa kwa siri.

Viongozi wa mashtaka wanasema watoto waliandikishwa kama askari , kuwauwa watu wa kabila lingine na pia kumlinda bwana Lubanga.

Bwana Moreno- Ocampo alisema wana ushahidi kwamba kati ya Tarehe 1 Septemba 2002 na tarehe 13 Agosti mwaka 2003 bwana Lubanga aliwaandikisha watoto wa chini ya miaka 15 kuwa wanajeshi.

Amesema baadhi ya watoto hao mpaka leo wameathirika kutokana na yale waliyoyaona na kuyafanya, na kwamba wengine sasa wanatumia dawa za kulevya na kujiingiza katika ukahaba ili kujikimu.

Viongozi wa mashtaka wanakusudia kuleta mashahidi 34 , miongoni mwao watoto waliotumikishwa jeshini na wapiganaji waliojisalimisha. Kesi hii inatarajiwa kuchukua muda wa miezi kadhaa.

Sehemu ya ushahidi ni kanda ya Video inayodaiwa kumwonyesha Bwana Lubanga akiwa katika kambi za kutoa mafunzo ya kijeshi akiandamana na wanajeshi wanaoonekana wazi kuwa watoto wa chini ya umri wa miaka 15.

Bwana Lubanga anasisitiza kuwa alikuwa anajaribu kuleta amani katika eneo la Ituri - mashariki mwa Congo, ambako kumekuwa na mzozano wa miaka mingi baina ya makundi mbali mbali yanayotaka kudhibiti madini mengi yanayopatikana huko.

Lubanga alikuwa kiongozi wa kundi la Union of Congolese Patriots (UPC) na kitengo cha kijeshi cha kundi hilo, wakati ambapo uhalifu huo unadaiwa ulifanyika kati ya mwaka 2002-2003 , na bado ana wafuasi kutoka jamii ya waHema inayopatikana Ituri.

Zaidi ya watoto 30,000 waliandikishwa katika mapigano hayo, ambapo watu 60,000 walipoteza maisha.

Mwandishi wa BBC Kesi hiyo ni onyo kubwa kwa viongozi wa waasi na makamanda wa kijeshi kote duniani ambao mara kwa mara wameweza kufanya uhalifu wakiwa vitani bila kujali .


Source: BBC

No comments:

Post a Comment