Tuesday, January 6, 2009

Kili Stars yaifunga Zenji

Timu ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, jana ilifanya kweli baada ya kuwakandamiza ndugu zao wa Zanzibar, Karume Boys, kwa bao 2-1, katika mchezo wa michuano ya Kombe la Chalenji uliofanyika kwenye uwanja wa Nakivubo mjini hapa.

Kwa ushindi huo, Kili Stars sasa imefikisha pointi tatu huku Zanzibar wakiwa na nne lakini wamecheza mechi tatu ikiwa ni moja zaidi ya Bara.

Kilimanjaro Stars ilipata bao la kuongoza katika dakika ya 13 lililowekwa kimiani na Danny Mrwanda aliyefunga kwa kichwa akiunganisha mpira uliopigwa na Kigi Makasi.

Zanzibar ilisawazisha katika dakika ya 21 kwa bao lililofungwa na beki wa Yanga na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Nadir Haroub Canavaro kwa kichwa akiwahi krosi iliyochongwa na Abdi Kassim.

Mrwanda nusura aipatie Kili Stars bao jingine katika dakika ya 22, lakini alishindwa kufunga licha ya kuwa katika nafasi nzuri, ambapo alipiga shuti lililodakwa na kipa Mohamed Abdallah.

Mohamed Seif aliikosesha Zanzibar bao katika dakika ya 60 kufuatia mpira wa kichwa alioupiga kutoka nje wakati tayari kipa Juma Dihile akiwa amepotea mwelekeo.

Kili Stars ilijihakikishia ushindi kwa bao lililofungwa na mchezaji wa Yanga Athumani Idd Chuji katika dakika ya 78 baada ya kupiga mpira wa adhabu uliokwenda moja kwa moja wavuni na kuandika bao la pili.

Adhabu hiyo ilitolewa na mwamuzi Ali Farah baada ya Mrwanda kuchezewa vibaya na mchezaji mmoja wa Zanzibar.

Kocha wa Kili Stars, Mbrazil Marcio Maximo alisema kuwa mchezo huo ulikuwa mgumu kama alivyosema awali na ilitokana na Zanzibar kuwa na beki imara, na baada ya Zanzibar kusawazisha, wachezaji wake walikosa nguvu, lakini kipindi cha pili walibadilika na kupata bao la ushindi.

Naye kocha msaidizi wa Zanzibar, Hafidh Badru alisema mwamuzi aliiuma timu yake na kuipendelea Bara na kuwafanya wachezaji wa timu hiyo kupoteza umakini.

Timu zilikuwa;Zanzibar:Mohamed Abdallah, Haji Abdi. Omar Juma/Ali Hamza (58), Nadir Haroub Canavaro, Suleiman Kassim, Mohamed Seif, Haji Ramadhani, Amour Suleiman, Abdi Kassim , Aggrey Morris na Abdughani Gulam.

Kili Stars:Juma Dihile, Shdrack Nsajigwa, Juma Jabu, Meshack Abel, Salum Sued, Godfrey Bonny, Mrisho Ngassa, Henry Joseph/Athuman Idd (dk.57), Danny Mrwanda, Haruna Moshi Boban na Kigi Makasi/Mussa Hassan Mgosi (dk.58)

Katika mchezo wa kwanza jana, Rwanda waliikandamiza Somalia 3-0. Somalia iliifunga Bara 1-0 katika mchezo uliofanyika Jumamosi.

Mashindano hayo yanaendelea tena leo kwa Kenya kucheza na Djibout, huku Burundi wakipepetana na Sudan.



Source: Nipashe

No comments:

Post a Comment