Friday, January 23, 2009

Pemba sasa yamkuna Kikwete

RAIS Jakaya Kikwete ameridhishwa na mabadiliko ya kisiasa yanayoendelea sasa katika kisiwa cha Pemba na kuwataka wananchi wake kuendelea na hali hiyo, kwa sababu kwenye siasa kila mmoja ana utashi wake, lakini siasa si uadui.

Akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara wa wananchi kwenye Uwanja wa Gombani ya kale mjini Chake Chake juzi, Rais Kikwete alisema amevutiwa na hali ya mabadiliko hayo yanayojitokeza sasa na akasema hiyo ni ishara nzuri kwa wananchi wa kisiwa hicho kilichogubikwa na siasa tete kwa miaka kadhaa.

Alisema katika siasa kila mtu ana utashi wake, lakini siasa si uadui, na kwamba wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wa Chama cha Wananchi (CUF), wanapaswa kushirikiana kila baada ya uchaguzi kumalizika.

“Muige mfano wa ushabiki wa Simba na Yanga, wao wanashindana na kubishana wakati wa mechi, na inapomalizika wanarudi kuwa kitu kimoja hata kama mmoja wao ameshindwa. Mwingine anasubiri raundi ijayo. Mngetumia mithili hiyo, ukishindwa leo, unasubiri wakati mwingine,” alisema Rais na kuongeza:

“Mabadiliko hayo yanaashiria mambo mema, kwa hiyo kwa viongozi wenzangu wanaomba watazame matendo yao kwa sababu haya (ya vurugu) yanatokea kwa sababu ya matendo ya viongozi.

Tusiwapeleke wanachama wetu kusikotakiwa.” Aliwataka wananchi hao ambao wengi walikuwa ni wanachama wa CCM na wananchi wa mikoa miwili ya Kusini Pemba na Kaskazini Pemba, kukijenga kisiwa chao kwa kushirikiana na kusahau matatizo yao mara tu uchaguzi unapomalizika.

Alisema hilo litasaidia kuwavutia wawekezaji kuweka miradi yao katika kisiwa hicho kwa sababu watahakikishiwa usalama wa mali zao, tofauti na miaka ya karibuni, hali ilipokuwa tete kutokana na mzozo wa kisiasa baina ya vyama hivyo viwili vikuu, kiasi cha watu kutozikana, kutosalimiana na kuchomeana nyumba. Kwa upande wake, Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha, alisema hali anayoiona sasa inaashiria mazuri kwa siku za usoni kwa kisiwa hicho na Chama Cha Mapinduzi kwa ujumla.

Aliwataka wana-CCM kutovunjika moyo kwa sababu wapo watu wenye mioyo migumu katika kukubali jambo, lakini SMZ itaendelea kuwapelekea maendeleo wananchi wa kisiwa hicho hata kama hawaoni jitihada zinazofanyika. “Naona mwanga wa matumaini, nitashangaa sana kama mwaka 2010 kama mioyo migumu haitalainika,” alisema Nahodha.

Naye mke wa Rais Kikwete, Salma aliwataka vijana wapatao 235 ambao walijiunga na CCM wakiwamo 65 kutoka vyama vya upinzani, kutoogopa na kutishwa, badala yake wawe mstari wa mbele kuitetea CCM. Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Saleh Ramadhan Ferouz alisema mahali pasipo na amani uchumi unadidimia, hivyo akawataka wananchi wa Pemba kudumisha amani ili kuvutia wawekezaji.

Alimpongeza Rais Kikwete na Rais Amani Abeid Karume kwa ushirikiano wa pamoja uliosaidia kuleta maendeleo kwa wananchi wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment