WEKUNDU wa Msimbazi, Simba Sports Club, jana walifanikiwa kukamata nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya Bara kwa kufikisha pointi 23, baada ya kuwamenya maafande wa Prisons ya Mbeya kwa mabao 3-1.
Matokeo ya mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam yameiwezesha Simba kufikisha idadi hiyo ya pointi kama ilivyo kwa Kagera Sugar.
Hata hivyo, Simba ni ya pili kutokana na mabao mengi ya kufunga. Kagera Sugar imefikisha pointi 23 huku ikifunga mabao 14 wakati Simba imezifumania nyavu mara 19.
Kwa matokeo hayo, Simba imezipiga kumbo Kagera Sugar iliyokuwa ikikamata nafasi ya pili kabla ya mechi ya jana, na Mtibwa Sugar iliyokuwa nafasi ya tatu.
Katika mechi hiyo ya jana, Simba walio chini ya Kocha Mzambia, Patrick Phiri na wakionekana kukamia, walicheza soka ya nguvu kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mechi hiyo.
Licha ya Prisons - wawakilishi wa Tanzania Bara katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF) - kuonyesha uhai katika kipindi cha kwanza, katika kipindi cha pili, walionekana kuelemewa na zigo la kandanda safi ya Wekundu hao wa Msimbazi.
Simba ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya pili ya mchezo, likifungwa kiufundi na mchezaji machachari, Adam Kingwande, baada ya kupokea krosi iliyomiminwa na Said Nassor ‘Cholo’. Kingwande alisukuma kiki ya kimo cha ng’ombe mzee iliyokwenda wavuni dairekti huku ikimuacha kipa wa Maafande hao akigaagaa chini.
Bao hilo lilionekana kuwaamsha maafande wa Prisons walioanza kupanga mashambulizi. Walifanikiwa kusawazisha bao katika dakika ya 27 likifungwa na Yona Ndabila kutokana na krosi ya Ramadhani Katamba.
Katika dakika ya 31 Simba walipata bao pili kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa na mwamuzi, Ahmad Kikumbo, wa Dodoma baada ya Jabir Aziz kuangushwa ndani ya maguu 12.
Mussa Hassan Mgosi hakufanya makosa - akaukwamisha mpira wavuni akimwacha kipa Nelson Kimath akichupa bila mafaniko, alipodanganyika kufuata ngoma upande sio. Hadi mapumziko Simba walikuwa mbele kwa mabao 2-1.
Simba walikianza kipindi cha pili cha mchezo wa kasi, hivyo kuwachukua dakika nne tu kupiga bao la tatu, safari hii likifungwa na Emeh Izechukwu.
Ni bao lililotokana na mpira wa kurushwa na Cholo na kutua kichwani kwa Izechukwu, hata hivyo kipa akapangua na kumfikia Izechukwu ambaye alifunga kwa kichwa.
Licha ya maafande wa Prisons kupigana vilivyo kusawazisha mabao hayo, lakini hadi filimbi ya mwisho, Simba walikuwa kidedea kwa mabao 3-1.
Kocha wa Prisons, James Nestory, alisema kipa wake kutokuwa makini kumeigharimu timu, kwani wachezaji wa ndani walicheza vizuri.
Naye Patrick Phiri alisema anashukuru kushinda mechi ya jana kwani ilikuwa ngumu na kwamba nia yake ni kumaliza ikiwa nafasi ya pili.
Aidha, licha ya kukamata nafasi ya pili Simba haina ubavu wa kutwaa ubingwa kwani hata ikishinda mechi zote nane zilizosalia, inaweza kufikisha pointi 47. Wakati Simba wakiishia hapo, mtani wake, Yanga, naye kama atashinda zote, anaweza kufikisha pointi 63.
Aidha, kama Kagera Sugar itashinda mechi zake zote itafikisha pointi 47 huku Mtibwa Sugar ikiwa na ubavu wa kufikisha pointi 45. Kwa vile ubavu wa Simba na Kagera Sugar ni kufikisha pointi 47, hivyo Yanga imebakisha pointi 9 tu kutwaa ubingwa.
Kama itashinda mechi hizo tatu dhidi ya Moro United, Polisi Moro na Toto Africa Yanga itakuwa imetwaa ubingwa huku ikiwa imesaliwa na mechi tano mkononi, kama ilivyowahi kufanya chini ya makocha Sunday Kayuni na Tito Mwaluvanda (marehemu).
No comments:
Post a Comment