Wednesday, January 14, 2009

Stars yalinda heshima, yashinda 3-2

TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’, angalau jana iliwafariji Watanzania baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Burundi hivyo kushika nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Chalenji iliyomalizika jana.

Mchezo huo wa kusisimua wa kutafuta mshindi wa tatu ulifanyika kwenye Uwanja wa Mandela nje kidogo ya mji wa Kampala, ambapo hadi mapumziko Burundi ilikuwa mbele kwa mabao 2-1.

Stars inayonolewa na Mbrazili Marcio Maximo ilitangulia kupata bao dakika ya pili, mfungaji akiwa Mrisho Ngasa, lakini kabla hata watazamaji hawajatulia vizuri vitini, Burundi ilisawazisha dakika ya tano kwa mkwaju wa penalti.

Penalti hiyo ilitolewa baada ya Henry Joseph kumuangusha Nahimana Claude katika eneo la hatari, ambapo Irambona Abdallah alipachika wavuni penalti hiyo. Warundi ambao katika nusu fainali walinyukwa mabao 5-0 na Uganda, walipachika bao la pili dakika ya 42, mfungaji akiwa Jaffar Jumapili kwa shuti.

Jerry Tegete aliyeingia kipindi cha pili alipachika bao la pili dakika ya 68, kabla Danny Mrwanda kupachika bao la tatu dakika ya 76.

No comments:

Post a Comment