Saturday, January 10, 2009

Kilimanjaro Stars yafungwa, yaingia nusu fainali

Licha ya kufungwa mabao 2-1 na Uganda ‘The Cranes’ jana, timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ imefuzu nusu fainali ya michuano ya Kombe la Chalenji.

Stars jana ilifungwa mabao hayo katika mchezo wa mwisho wa Kundi A uliofanyika Uwanja wa Nakivubo mjini Kampala, ikiwa ni muda mfupi baada ya ndugu zake wa Zanzibar kufungwa mabao 3-0 na Rwanda katika mchezo mwingine wa kundi hilo.

Kwa mazingira hayo, Stars imemaliza michuano hiyo ikiwa na pointi sita kama ilivyo Rwanda, lakini Stars ina uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa, ambapo Stars imefunga mabao matano na kufungwa manne, huku Rwanda ikiwa imefungwa mabao sita na kufunga sita.

Rwanda ilifungwa mabao 4-0 na Uganda, kisha ikachapwa mabao 2-0 na Stars, wakati yenyewe Stars jana ilifungwa mabao 2-1, kisha iliifunga Zanzibar mabao 2-1 na ilifungwa na Somalia bao 1-0. Kutokana na matokeo hayo, Stars sasa imeshika nafasi ya pili katika kundi hilo na itacheza na Kenya iliyoshika nafasi ya kwanza Kundi B.

Uganda iliyoshika nafasi ya kwanza Kundi A ikiwa na pointi 10, baada ya kushinda michezo mitatu na kutoka sare mmoja, itacheza na mshindi wa pili Kundi B Burundi. Katika mchezo wa jana, Uganda ilipata bao dakika ya 11 mfungaji akiwa Omony Bryan aliyewatoka mabeki wa Stars na kutumbukiza mpira wavuni, kabla ya Stephen Bengo kuongeza la pili dakika ya 27 kutokana na mpira wa kona.

Kipindi cha Stars kilianza kwa kasi zaidi, ambapo dakika ya 48 Stars ilipata bao mfungaji akiwa Salum Sued kwa mkwaju wa penalti baada ya Danny Mrwanda kuangushwa alipokuwa akielekea kufunga. Kilimanjaro Stars ilipata pigo dakika ya 87 baada ya Kelvin Yondani kuonyeshwa kadi nyekundu akidaiwa kumpiga Omony Bryan.

Kilimanjaro Stars:Deo Bonaventura, Shadrack Nsajigwa, Juma Jabu, Said Sued, Kelvin Yondani, Henry Joseph (Nurdin Bakari dk.62), Mrisho Ngassa (Mussa Hassan `Mgosi\' dk.77), Godfrey Bonny, Danny Mrwanda, Haruna Moshi `Boban\'(Nizar Khalfan dk.86) na Athumani Iddi `Chuji`.

Mchezo wa mapema jana, Rwanda iliifunga Zanzibar mabao 3-0 yaliyofungwa na Lomani Jean dakika ya 11, Hakiri Jean dakika ya 17 na Gasana Jean Bosco dakika ya 39.

Akizungumza baada ya mchezo huo, kocha wa Zanzibar, Mmisri Badr El-Din alidai kuwa wachezaji wake walicheza kwa hofu ndio maana walijikuta wakiboronga.

Kocha wa Rwanda, Branco Tucak alisema ari ya wachezaji ndio iliyowasaidia baada ya kupoteza mechi zao kwa Uganda na Tanzania Bara.

No comments:

Post a Comment