Monday, January 19, 2009

Simba yatwaa pointi tatu kwa Polisi Moro

SIMBA jana ilianza vyema mzunguko wa pili wa ligi kuu Tanzania Bara, kwa kuifunga Polisi Morogoro kwa mabao 3-2. Ushindi huo ni mwanzo mzuri kwa kocha mpya wa timu hiyo, Patrick Phiri, na pia umetimiza dhamira ya timu hiyo ya kutaka kushinda mechi zote za mzunguko wa pili. Hata hivyo mchezo huo umedhihirisha kuwa kocha Phiri bado ana kazi kubwa ya kuunoa mstari wa ushambuliaji, ambao ulipoteza nafasi nyingi.

Mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ulishuhudia Simba ikibisha hodi langoni kwa wapinzani wao dakika ya sita, kupitia kwa Mussa Hassan 'Mgosi' aliyekosa bao la wazi baada ya kubaki na kipa.Simba iliendelea kufanya mashambulizi langoni mwa wapinzani wao, ambapo dakika ya tisa Nico Nyagawa alipata nafasi ya kufunga, lakini shuti kali alilopiga lilipaa hewani.

Dakika ya 33 Mgosi alipata nafasi nyingine ya kufunga baada ya kupokea pasi safi ya Nyagawa, lakini mabeki wa Polisi walikuwa makini kuokoa hatari hiyo.Polisi ilijibu mashambulizi hayo kwa kufanya mashambulizi ya kustukiza langoni kwa Simba, lakini mabeki Kevin Yondan na Juma Nyoso waliondoa hatari hizo.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika timu zote zilienda mapumziko zikiwa hazijaona lango la mwenzake.Kipindi cha pili kilipoanza, Simba ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Adam Kingwande na nafasi yake kuchukuliwa na Orji Obinna, aliyewanyanyua mashabiki wa timu yake vitini.Alifunga bao la kwanza dakika nne tu tokea kipindi hicho kianze kwa kuunganisha pasi ya Nyagawa.

Dakika tatu baadae, Polisi ilisawazisha bao hilo kupitia kwa Nico Kabipe, aliyefunga kwa kichwa baada ya mabeki wa Simba na golikipa wake Deo Bonventure, kuchanganyana. Kufuatia bao hilo, timu zote zilizidisha mashambulizi na dakika ya 61 Simba iliandika bao la pili kupitia kwa Obinna, aliyepokea pasi ya Mgosi.

Hata hivyo, funga nikufunge iliendelea kwani bao hilo halikudumu, na dakika ya 71 Ally Moshi aliyetokea benchi aliisawazishia Polisi kwa kuweka wavuni bao la pili. Baada ya bao hilo, Polisi ilijizatiti na kufanya mashambulizi ya hapa na pale, ila umaliziaji mbovu uliifanya timu hiyo kukosa mabao ya wazi.Mgosi alifunga bao la tatu dakika ya 75, baada ya kupokea pasi ya Nyagawa, na kuifanya timu yake kuibuka na ushindi katika mchezo huo.

Licha ya Simba kuibuka mshindi katika mchezo huo, timu hiyo haikuweza kuonyesha kandanda safi baada ya wachezaji wake kuonekana kutoelewana, na wakikosa mabao mengi ya wazi kupitia kwa Mgosi.Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Phiri, alisema licha ya timu yake kushinda, mchezo ulikuwa mgumu kwa timu yake.

Phiri alisema baada ya mchezo huo anatarajia kukifanyia marekebisho kikosi chake kwa ajili ya kujiandaa na mchezo mwingine dhidi ya Villa Squad, utakaofanyika keshokutwa.

Simba ilipangwa hivi: Deo Bonventure, Juma Jabu, Kevin Yondan, Henry Joseph, Juma Nyoso, Said Nassor, Jabir Aziz, Adam Kingwande/Obinna, Mgosi na Nico Nyagawa.

Polisi Morogoro: Benjamin Haule, Nahoda Bakari, Haji Mbelwa, Juma Mkeketa/Tofaya Daud, Seleman Kissi, Adam Juma, Delta Thomas, Fred Agai/Thobias John, Mokati Lambos/Ally Moshi, Sammy Kessy na Nico Nabipe.

No comments:

Post a Comment