Wednesday, January 28, 2009

Yanga njia nyeupe kileleni

Mabingwa wa soka Tanzania Bara Yanga jana waliendeleza makali kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Bao hilo pekee katika mchezo huo lililoiwezesha Yanga kufikisha pointi 39, liliwekwa kimiani na Mrisho Ngassa dakika nane tangu kuanza kwa mchezo huo akiunganisha wavuni krosi ya Mkenya Ben Mwalala.

Licha ya Yanga kutawala mchezo huo, kocha wao Mserbia Dusan Kondic aliwalalamikia waamuzi na kusema kuwa wanachangia kwa kiasi kikubwa alisema kuwa waamuzi wamekuwa wakichangia sana kurudisha nyuma soka la bongo kwa kutotoa maamuzi sahihi na badala yake kupendelea.

Naye kocha wa Mtibwa Sugar Salum Mayanja alisema kuwa mchezo ulikuwa mgumu kwao kama alivyotegemea, lakini waliangushwa na viungo na washambuliaji wake kwa kutokuwa makini, hivyo atawanoa zaidi.

Timu zilikuwa Yanga:Obren Curkovic, Shadrack Nsajigwa, Nurdin Bakari, Nadir Haroub `Canavaro`, Wisdom Ndlovu, Godfrey Bony, Mrisho Ngassa, Athuman Idd Chuji/Mike Baraza )dk.47), Boniface Ambani/Amir Maftaha (dk. 83), Ben Mwalala/Abdi Kassim (dk.57) na Shamte Ally.

Mtibwa Sugar:Shaban Kado,Mecky Maximo, Idrisa Rajab, Chacha Marwa, Salum Sued, Shaban Nditi, Zahoro Pazi/Omary Matuta (dk. 62), Rashid Gumbo, Abdallah Juma/Salum Ussi (dk. 74), Uhuru Suleiman na David Mwantobe/Yussuf Mgwao (dk.41).

Mwandishi Wetu anaripoti kuwa; timu ya Simba leo inashuka kwenye uwanja huo wa taifa kukwaruzana na Prisons ya Mbeya katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mechi hiyo ambayo itakuwa ni ya tatu kwa kocha mpya wa Simba, Patrick Phiri tangu arejee tena Msimbazi, inatarajiwa kuwa na ushindani kutokana na historia ya timu hizo zinapokutana katika mechi za ligi.

Ushindi kwa Simba ambayo iko katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ni muhimu kutokana na kutaka kurejesha matumaini ya kushiriki katika mashindano ya kimataifa mwakani na itakuwa imeweza kupanda hadi katika nafasi ya pili.



Source: Nipashe

No comments:

Post a Comment