Sunday, February 1, 2009

Yanga yawachanachana Wacomoro

Yanga jana iliingia raundi ya pili ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika ambako itakutana na mabingwa watetezi National Al Ahly ya Misri baada ya kuichabanga Etoile d`Or Mirontsy ya Comoro kwa magoli 8-1 katika mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza kwenye Uwanja wa Taifa, Boniface Ambani akiona nyavu mara nne.

Yanga ilipata bao la kwanza katika dakika ya pili lililofungwa na Ambani kwa shuti kali lililomshinda mlinda mlango Maudese Mohamed.

Lakini katika mchezo ambao mshindi baada ya mechi ya marudiano atakumbana na bingwa mara sita wa Afrika Al Ahly, d'Or Mirontsy ilisawazisha katika dakika ya 20 kupitia kwa Aboubakar Alisoul aliyesindikizwa na walinzi wa Yanga na kosa la Juma Kaseja kutoka langoni mapema.

Itakuwa ni ajabu kama Yanga sasa itatolewa baada ya ushindi huo mkubwa licha ya ukweli kuwa itakabiliwa na tatizo la dharau pindi itakapokuwa ugenini wiki mbili zijazo.

Jerson Tegete aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Benard Mwalala alipachika bao la pili kwa shuti la nguvu katika dakika ya 54 baada ya kuwahi mpira uliopigwa na Ambani.

Dakika 16 baadaye Ambani aliongeza bao la tatu kwa penalti iliyotolewa na mwamuzi kutoka Uganda baada ya Mrisho Ngassa kufanyiwa madhambi na mmoja wa walinzi wa Etoile.

Mlinzi Wisdom Ndlove alipachika bao la nne kwa kichwa baada ya kuwahi mpira wa kona uliopigwa na Abdi Kassim katika dakika ya 74, na dakika mbili baadaye Tegete tena alipachika bao la tano baada ya kupokea pasi murua ya Vicent Barnabas aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Kigi Makassy.

Ambani ambaye ni kinara wa magoli katika ligi kuu akiwa amefunga magoli 13 hadi sasa alipachika bao la sita baada ya kupata pasi kutoka kwa Ngassa katika dakika ya 79, na dakika mbili baadaye Ngassa aliongeza bao la saba kwa shuti na Ambani alifunga kitabu cha magoli katika dakika ya 85 kwa kufunga bao la nane.

Kocha wa Yanga Dusan Kondic aliwapongeza wachezaji wake kwa kujua majukumu yao hasa katika kipindi cha pili na kusema pia hatadharau mchezo wa marudiano.

Naye kocha wa Etoile, Nasurdine Maanrouf alisema timu yake haina uzoefu katika michuano ya kimataifa na hii ni mara yao ya kwanza kushiriki.

Timu zilikuwa:
Yanga: Juma Kaseja, Shadrack Nsajigwa, Amir Maftaha, Nadir Haroub `Canavaro`, Wisdom Ndlove, Geofrey Bonny (Nurdin Bakari dk.44), Mrisho Ngassa, Abdi Kassim `Babi`, Boniface Ambani, Benard Mwalala (Jerson Tegete dk.46) na Kigi Makassy (Vicent Barnabas dk.55).

Katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho, Mundu ilifungwa mabao 6-0 na Red Arrows ya Zambia katika pambano lililofanyika mjini Lusaka jana Jumamosi, habari kutoka Zanzibar zilisema jana.

Wawakilishi wa Zanzibar katika michuano kama ya Yanga, Miembeni itacheza leo na Monomotapa ya Zimbabwe ugenini.




Source: Lete Raha

No comments:

Post a Comment