Monday, February 2, 2009

Theluji nzito yavuruga usafiri London

Usafiri wakwama London kutokana na theluji nzito

Maelfu ya wakaazi wa London wameshindwa kwenda kazini leo kutokana na theluji nzito iliyoanguka usiku kucha na usafiri wa mabasi na treni kutatizika na theluji inaendelea kuanguka.

Usafiri wote wa mabasi na treni ziendazo chini ya ardhi hasa Circle, Hammersmith & City na Waterloo & City zimesimamishwa.

Njia zote za kurukia ndege isipokuwa moja tu katika uwanja wa ndege wa Heathrow zimefungwa. Uwanja wa ndege wa London bado umeendelea kufungwa.

Theluji hiyo nzito imesababisha ndege ya shirika la ndege la Cyprus kuteleza na kutoka katika njia wakati ikielekea kuegesha katika uwanja wa Heathrow na ikajikita katika eneo la nyasi.

Kwa mujibu wa Mamlaka inayosimamia uwanja wa ndege wa Heathrow abiria wote walikuwa salama katika tukio hilo lililotokea mapema saa mbili na dakika ishirini asubuhi.

Mamlaka hiyo imearifu ndege hiyo ilikuwa ni ya mwisho kuwasili kabla sehemu za kurukia na kutua ndege hazijalazimika kufungwa.

Shirika la ndege la Uingereza-British Airways limesema limefuta safari zake zote za ndege hadi itakapofika saa kumi na moja jioni.

Kwa mujibu wa wataalam wa hali ya hewa hali kama hii ya kuanguka theluji nzito haijawahi kulikumba jiji la London kwa miaka 18 iliyopita.



Source: BBC

No comments:

Post a Comment