Friday, February 20, 2009

Stars Yatua Salama Abidjan, Wa Kwanza

Zikiwa zimesalia saa kadhaa kabla ya vumbi la fainali za michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (CHAN), kuanza kutimka nchini Ivory Coast Jiji la Abidjan limegubikwa na shamrashamra za ufunguzi wa michuano hiyo.

Michuano hiyo imeundwa maalumu kwa ajili ya wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani kwenye mataifa yao, imekuwa gumzo kubwa katika jiji hilo la kibiashara la taifa hilo la Afrika Magharibi.

Kutoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Felix Houphoet Boigny mpaka maeneo ya Adjame, Treichville na kwingineko katika Jiji hilo la Abidjan kuna mabango ya matangazo yenye kuitangaza michuano hiyo mipya iliyoandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).

Ukifika katika Mji Mkuu huo wa Ivory Coast, ambao ni mojawapo ya miji ambayo itakuwa wenyeji wa michuano hiyo, ambayo inaanza Februari 22 na kumalizika Machi 8, utabaini joto la homa na mshawasha wa michuano hiyo kwa mashabiki wa soka wa taifa hilo liko juu na wanasubiri kwa hamu kubwa ufunguzi wake.

Mara tu utakapowasili kwenye Uwanja wa Ndege utakaribishwa na mandhari nzuri ya mabango ya umeme yaliyopambwa ndani ya kiwanja wakati ukiendelea kukamilisha taratibu za kuingia katika nchi hiyo. Hata vigari vya kubebea mizigo uwanjani hapo vimepigwa chapa yenye nembo inayotambulisha michuano mipya ya CHAN.

Vyombo vya habari vyote vya nchi hiyo, magazeti na televisheni pia haviko nyuma kutokana na habari kwenye vyombo hivyo kutawaliwa zaidi na habari za michuano hiyo mipya kwenye kalenda ya Caf. Timu za mataifa nane ikiwamo, Ivory Coast ambao wamefuzu kucheza fainali hizo kutokana na kuwa wenyeji zitakuwa zikichuana vikali kuwania taji hilo jipya.

Timu nyingine kwenye michuano hiyo ni Libya ( kutoka Kanda ya Kaskazini mwa Afrika), Ghana (Kanda ya Magharibi B), Senegal (Kanda ya Magharibi A), Tanzania (Kanda ya Kati) na Mashariki, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Kanda ya Kati) na Kanda ya Kusini ni Zambia na Zimbabwe. Kundi A la michuano hiyo, ambalo litakuwa likichezea mechi zake katika Jiji la Abidjan linaundwa na wenyeji Ivory Coast , Senegal, Tanzania na Zambia, wakati lile la B lina timu za Ghana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Libya na Zimbabwe.


No comments:

Post a Comment