Thursday, February 26, 2009

Taifa Stars yawapa raha Watanzania yawaondoa wenyeji Ivory Coast

Mrisho Ngasa ndiye aliyepachika bao la ushindi baada kupokea mpira kutoka kwa Henry Joseph.

TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imefufua matumaini ya kuingia nusu fainali ya Fainali za Afrika kwa wachezaji wa Ligi za Ndani, CHAN baada ya kuifunga Ivory Coast bao 1-0, mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Felix Houphouet Boigny, mjini Abidjan jana.

Matokeo hayo yamewaondosha kabisa wenyeji katika michuano hiyo, sasa watacheza na Senegal Jumamosi, mchezo wa kukamilisha ratiba katika mchezo wa kwanza walifungwa mabao 3-0 na Zambia.

Stars bado iko katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi tatu wakati Zambia inaongoza ikiwa na pointi nne sawa na Senegal lakini Zambia ina mabao mengi. Wenyeji wanashika mkia kwa kutokuwa na pointi.

Ili kusonga mbele, Stars inahitaji ushindi dhidi ya Zambia Jumamosi huku ikiombea Ivory Coast kumfunga Senegal ili kujihakikishia nafasi nzuri zaidi.

Ukiacha hayo, katika mchezo wa jana, wenyeji walianza kwa kasi na kuanza kushambulia mfululizo lango la wapinzani wao, lakini hata hivyo, ngome ya Stars chini ya Shadrack Nsajigwa, Salum Swed, Juma Jabu na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ walisimama imara kupunguza kasi ya mashambulizi.

Kasi ya wenyeji iliwachanganya mara kwa mara Stars hata kuruhusu kona 17, nane zikipigwa kipindi cha kwanza huku wenyewe wakiambulia nne kipindi cha pili na kipindi cha kwanza hawakupata kona.

Kiujumla Ivory Coast walifanya mashambulizi mengi wakiongozwa na Junior Mango, Sanny Karamoko na Silvestre Nene lakini hata hivyo hayakuwa na madhara kutokana na ukuta imara wa Tanzania.

Stars ambayo ilichapwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza na Senegal, walionyesha kubadilika lakini pengine ni kutokana na kubadilisha kikosi kwa kumuanzisha Mussa Hassan Mgosi na Kigi Makassi.

Kocha wa timu hiyo, Marcio Maximo alimtema kikosini Haruna Moshi ‘Boban’ pamoja na Athumani Idd ‘Chuji’ ambao hata hivyo, Mwananchi ilifuatilia na kugundua kuwapo na ‘bifu’ la chini kwa chini kati ya Boban na Maximo wakati Chuji alijitonesha mazoezini.

Wachezaji hao wote walikuwa jukwaani na hawakuwa hata katika benchi la ufundi.

Watanzania walishangilia kwa nguvu katika dakika ya 38 wakati Mrisho Ngassa alipopachika bao kwa kichwa baada ya kupata pande la mbali la Henry Joseph kutoka katikati ya uwanja.

Stars iliyokuwa ikishambulia kwa kushtukiza, waliliandama lango la wapinzani wao kipindi cha kwanza huku Mussa Hassan Mgosi, Ngassa wakiwatesa wenyeji kwa kuunganishwa na Henry Joseph, Kigi Makasi na Nizar Khalfan.

Hata hivyo, Henry na Nizar walionekana kupwaya kwa vipindi hata kupoteza mipira mfululizo. Kipindi cha pili, Maximo alifanya mabadiliko kadhaa, aliwatoa Henry Joseph, Mussa Hassan Mgosi na Mrisho Ngassa na nafasi zao kuchukuliwa na Mwinyi Kazimoto, Shaaban Nditi na Jerry Tegete lakini hata hivyo sura ya mchezo haikubadilika.

Stars iliwakilishwa na Juma Dihile, Shadrack Nsajigwa, Juma Jabu, Said Sued, Nadir Haroub, Nurdin Bakari, Henry Joseph/Shaaban Nditi, Nizar Khalfan, Mussa Hassan Mgosi/Mwinyi Kazimoto, Mrisho Ngassa/Jerry Tegete na Kigi Makassi.

Katika mchezo mwingine, Zambia na Senegal zilitoka suluhu katika mchezo uliokuwa na ushindani.


Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment